Na. Lorietha Laurence -
Maelezo,Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
(Uchukuzi) Mhandisi Dkt. Leornad Chamuriho ameupa siku mbili uongozi wa Bandari
unaosimamia Mita ya Kupimia mafuta nchini (Flow Meter) iliyoko Kigamboni jijini
Dar es salaam kuhakikisha kuwa unatoa taarifa ndani ya siku mbili kuhusu
hitilafu iliyojitokeza kwenye mfumo wa kufungua valvu za mita hiyo upande wa
umeme.
Aidha, ameuagiza uongozi huo kutoa taarifa kuhusu
hitilafu ya kamera 2 za usalama zilizoungua na kushindwa kufanya kazi kwa
takribani mwezi mzima.
Katibu Mkuu huyo ametoa maagizo hayo mara baada ya
kufanya ziara ya kushtukiza katika mita hiyo eneo la mji Mwema Kigamboni leo
jijini Dar es salaam na kubaini upungufu wa utendaji wa baadhi ya maeneo.
Maeneo hayo ni pamoja na kamera za kufuatilia
mwenendo wa usalama wa mita hiyo, valvu zilizoshindwa kufanya kazi upande
wa mfumo wa umeme hivyo kubakiwa na njia ya analoji kutokana na hali ya mvua
zilizokuwa zikiendelea kunyesha jijini Dar es salaam.
“Ifikapo Jumatatu nipatiwe taarifa kuhusu matengenezo ya
vifaa hivi, hatua zilizochukuliwa na mnieleze lini ukarabati wake utakamilika
pia ujenzi wa paa kuzuia athari ya mvua kwenye mita hii” amesema Dkt.
Chamuriho.
Ameongeza kuwa dhumuni la Serikali ni kuhakikisha vifaa
hivyo vinafanya kazi katika viwango vinavyostahili ili kulinda mapato
yanayotokana na mafuta yanayoingia nchini ili Serikali ipate kodi halali na
hivyo kuongeza mapato ya nchi na kuondoa malalamiko kwa wateja.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Ujenzi wa Mita hiyo
kutoka Mamlaka ya Bandari nchini Mhandisi Mary Mhayaya ameeleza kuwa
uharibifu wa vifaa hivyo umesababishwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni na
tayari vifaa hivyo vimeanza kukabarati.
" Kisichofanya kazi ni mfumo wa kufungua mafuta
upande wa umeme kwenye baadhi ya valve, upande wa analoji unafanya kazi vizuri
na kazi ya upakuaji mafuta kupitia mfumo wa analojia inaendelea kama
kawaida" Amesisitiza.
Amesema kuwa tayari wamemweleza mkandarasi
aliyefunga vifaa hivyo kuvifanyia marekebisho haraka iwezekanavyo.
Naye Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)
Hebel Mhanga amesema kuwa ofisi yake inajukumu la kuhakikisha inatoa huduma
sahihi kwa wateja wanaotumia mitambo hiyo iliyopo bandarini hapo na
Serikali inapata mapato kulingana na huduma iliyotolewa.
Mita ya Kupimia Mafuta yalnayoingia nchini iko katika
hatua ya majaribio kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo tayari meli tatu
zimefanyiwa majaribio ya upakuaji wa mafuta huku moja ikiwa imefanyiwa vipimo.
No comments:
Post a Comment