Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Serikali imetangaza rasmi alama za Jumuiya ya Afrika Mashariki zitakazotumika kwenye Ofisi za Serikali na katika shughuli zote rasmi za kiserikali.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Bi. Mindi Kasiga amezitaja alama hizo kuwa ni bendera ya Taifa,bendera ya Jumuia ya Afrika Mashariki, wimbo wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na wimbo wa Taifa.
Kasiga amewambia waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuwa, kuanzia sasa bendera ya Jumuiya hiyo itapepea sambamba na Bendera ya Taifa kwenye Ofisi zote za Serikali huku wimbo wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ukiimbwa sambamba na wimbo wa Taifa katika shughuli rasmi za serikali kuanzia ngazi za Halmashauri hadi Taifa, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Mkataba wa uanzishwaji wa jumuiya hiyo kifungu cha 7(a).
“Mkataba huu unasisitiza jumuiya hii kuwa jumuiya ya watu, hivyo watanzania watahusishwa katika hatua zote za mtangamano huo, pamoja na kushirikishwa kikamilifu katika hatua mbalimbali za jumuiya ili kujua madhumuni ya kunufaika na fursa mbalimbali zitakazaopatikana ndani ya Jumuiya hiyo”, alisema Bi. Kasiga
Aidha, matumizi ya alama hizi ni njia mojawapop ya kujenga uzalendo na kumfanya Mwananchi ajisikie kuwa sehemu ya ushirikiano huu, aliongeza Bi. Kisiga
Vilevile, taasisi binafsi zinaweza kutumia alama hizi, huku shule na vyuo vikisisitizwa kutumia alama hzi kama sehemu ya kuelimisha na kuhamasisha vijana kuhusu Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.Wizara ya Mambo ya Nje, na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaratibu upatikanaji wa sampuli ya alama hizo kwa gharama za taasis, wizara au Ofisi husika.
No comments:
Post a Comment