Friday, February 05, 2016
NISHA AIOMBA SERIKALI KUWAANGALIA WATOTO JICHO LA TATU
Na Lilian Lundo - Maelezo
05/02/2016
Msanii wa Filamu na Balozi wa kutetea watoto waishio katika mazingira magumu Salma Jabu (Nisha) ameiomba Serikali kuwaangalia watoto hao kwa jicho la tatu. Nisha aliyasema hayo wakati akikabidhiwa ubalozi wa kudumu wa kutetea watoto waishio mazingira magumu wa New Hope Family Group leo jijini Dar es Salaam.
“Watoto hawa wamekuwa rafiki zangu kwa muda mrefu, nimekuwa na huruma sana pale nilipowaona wanalala na njaa wakati watoto wengine wanakula na kusaza,” alisema Nisha. Nisha aliongeza kwa kusema ni wakati wa kuwafuta machozi na wao wajione ni moja ya jamii ya kitanzania, kwa yoyote mwenye nguo tatu basi nguo moja atoe kwa ajili ya watoto hao.
Pia muigizaji huyo ameiomba Serikali kuangalia watoto hao kwa jicho kubwa, kwani yapo mengi ambayo wanahitaji ikiwa pamoja na elimu ili waweze kujiepusha na makundi mabaya ya mitaani.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa New Hope Family Omary Kombe alisema si jambo la busara kumwita mtoto majina kama panya rodi na mbwa mwitu huku tukihubiri amani na upendo kwenye majukwaa ya siasa na nyumba za ibada.
Aidha, Kombe amesema kuwa, familia ya New Hope imemchagua Nisha kuwa Balozi wao kutokana na moyo wake wa upendo na huruma si tu kwa watoto waishio katika mazingira magumu bali kwa jamii ya watu maskini na wanyonge.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment