Friday, February 12, 2016

KATIBU MKUU TUCTA ASIFIA SHERIA ZA KAZI


Wajumbe wa Kikao cha Tathmini ya Utendaji kazi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi wakifuatilia uwasilishwaji wa mada toka kwa viongozi mbalimbali wakati wa Ufunguzi wa Kikao hicho kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (TUCTA) amezisifia sheria za kazi kwa kuwa zimesaidia kuleta mabadiliko katika Nyanja za utoaji wa haki kazini.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Nicholaus Mgaya wakati wa Kikao cha tathmini ya utendaji kazi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kilichofanyika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mgaya ameeleza kuwa, ujio wa sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6/2004 pamoja na Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7/2007 zimesaidia kuleta mabadiliko makubwa katika Nyanja za utoaji haki.

“Kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) yapo maeneo ya Sheria za Kazi ambayo kama wadau tunadhani ni lazima kufanya mabadiliko yenye tija kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi wa Mahakama hii ya Kazi ili haki ya kila upande iweze kupatikana kwa wakati”, alisema Mgaya.

Aidha, Mgaya amegusia baadhi ya changamoto zinazokwamisha katika kupata haki katika Mahakama ya Kazi ikiwemo uhaba wa Majaji na Wasajili katika Mahakama, Upotevu wa Mafaili, Uhamisho wa Majaji, Madalali wa Mahakama, Kukinzana kwa Maamuzi ya Mahakama pamoja na Upungufu wa vitendea kazi.

Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu Mhe. Abdallah Possi ameeleza kuwa Mahakama sio chombo cha kutafsiri sheria na kutoa haki tu, bali ni chombo pia cha kukuza uchumi.

“Mahakama inavyotatua migogoro inasababisha hali ya utulivu katika sehemu za kazi kwa sababu uchumi wa nchi hauwezi ukakua kama zile sehemu za uzalishaji zitakua na migogoro.”Alisema Possi.

Akiongea kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu, Mhe. Possi alisema kuwa Sheria za Kazi nchini zinakataza masuala ya unyanyapaa wa aina yoyote, hivyo Waajiri pamoja na Vyama vya Wafanyakazi havinabudi kuzingatia usawa kwa watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Aisha Nyerere amesema kuwa, Mahakama ya Kazi ina wajibu wa kutolea maamuzi mashauri ya kikazi yaliyofunguliwa.

Aidha, ameongeza kuwa Kanuni ya saba Kanuni ndogo ya Kwanza ya Tangazo la Serikali la 2009/2010 linaelekeza kuundwa kwa Kamati ya Utatu katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ambapo kamati hizo zinaundwa na Jaji, Msajili katika Mahakama ya kazi, Mwanasheria wa Serikali Mfawidhi au Mwakilishi wake, Wajumbe wawili katika Vyama vya Wafanyakazi, Wajumbe wawili kutoka Vyama vya Waajiri, Mawakili wawili kutoka Chama cha Mawakili wa Tanganyika na Kamishna wa Kazi.

Kikao cha Tathmini ya Utendaji kazi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi kilichofanyika leo kimeshirikisha wadau mbalimbali wa Sheria wakiwemo Majaji,Mawakili,Wasajili, Wenyeviti wa Vyama vya Wafanyakazi na Vyama vya Waajiri.








No comments:

Post a Comment