Na. Lilian Lundo – Maelezo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni ACP Christopher Fuime amewataka wananchi wa Mkoa wa Kinondoni kutoa malalamiko ya uhalifu vituo vya Polisi badala ya kulalamika matukio ya uhalifu katika vyombo vya habari.
Kamanda Fuime amesema hayo leo kwa njia ya simu mara baada ya baadhi ya wananchi kulalamika kwenye vyombo vya habari kwamba kuna ukabaji na uporaji unaofanyika katika daraja la Manzese wakati wa usiku.
“Hatuwezi kujua kama daraja hilo linatumiwa na vibaka kupora na kuwakaba kama wananchi hawajaripoti kwenye vituo vyetu juu ya uhalifu huo kwani hata tunapofanya doria hatujawai kukuta kundi la watu bali mtu mmoja mmoja ambao huwa ni wapita njia,” alisema Fuime.
Fuime aliongezea kwa kusema, licha ya daraja hilo kutumika kuvushia watu lakini pia mara nyingi daraja hilo limetumika kama sehemu ya utalii kwa watanzania hasa kutoka mikoani, hivyo hupenda kupiga picha na hata kuangalia mji kutoka darajani.
Aidha, Fuime amewataka wananchi kutoa taarifa haraka iwezekanavyo pale wanapofanyiwa uhalifu wa aina yoyote kwani inawapa urahisi Polisi kujua ni wapi pakuanzia kuliko kunyamaza kimya na kulalamika kwenye vyombo vya habari.
No comments:
Post a Comment