Tuesday, March 11, 2014

KITUO CHA OILCOM TAWAQAL 'CHAKUMBWA NA KASHFA' TENA

Singida,

Familia moja iliyokuwa safarini kueleka wilayani Rorya mkoani Mara kutokea Dodoma, imekwama mjini Singida kwa zaidi ya saa 12 baada ya kuuziwa petrol iliyochanganywa na maji na kusababisha injini zao za magari kushindwa kufanya kazi ’kunoki’

Tukio hilo limetokea juzi saa mbili asubuhi baada ya magari mawili aina ya noah yenye usaji T.585 CLZ na T.295 BAN, kudaiwa kujaza petrol iliyochanganywa na maji katika kituo cha mafuta cha Oilcom (Tawaqal) kilichopo karibu na kiwanja cha michezo cha Namfua mjini Singida.

Petrol hiyo iliyodaiwa kuwa na maji, ilileta uharibifu mkubwa katika magari hayo na kusababisha kushindwa kuendelea na safari.

Akizungumza na waandishi wa habari, kiongozi wa msafara ambaye ni mfanyabiashara wa Dodoma mjini, Nyihita Wilfred Nyihita, alisema wakati akijaza petrol hakulizima gari yake na hivyo kusababisha ghafla kuzimika lenyewe.

Baada ya tukio hilo,walihisi pengine kuna tatizo la nyaya,lakini baada ya kuita mafundi na kulikagua, walibaini kuwa wameuziwa petrol iliyochakachuliwa kuchanganywa na maji.

“Gari letu jingine T.295 BAN, nalo lilizimika baada ya kusogea kama hatua nne hivi. Tuliita polisi kushuhudia uchakajuaji huo mbele ya wahudumu waliotuuzia petrol hiyo,” alifafanua Bw. Nyihita.

Akieleza zaidi, Bw. Nyihita alisema wameandikisha maelezo kituo cha kati cha polisi mjini Singida sawia na wahudumu wa kituo cha mafuta cha Oilcom-Tawaqal, ambao walikiri mbele ya polisi kuwa petrol yao ilikuwa na maji.

“Kwa sababu tulikuwa tunasfirisha msiba Rorya, hatukutaka kupoteza muda, tuliuomba uongozi wa kituo hicho watutengenezee magari yetu na watupe shilingi milioni mbili,ili endapo magari yetu yataharibika njiani, tuweze kutengeneza”,aliongeza Bw.Nyihita.

Alisema uongozi huo ulikubali na wakaleta mafundi kutengeneza magari hayo, na kuhusu malipo ya fidia ya shilingi milioni mbili, wakaahidi kutuma kwa njia ua m-pesa.

“Muda mfupi baadaye, walibadilisha uamuzi na wakadai hawawezi kutoa fedha hiyo hadi hapo Ewura itakapowaeleza juu ya fidia”,alisema.

Wakati huo huo, meneja wa kituo hicho ambacho katika kipindi cha nyuma kilwahi kufungiwa na Uwura kutokana na kukiuka taratibu, alikataa kutaja jina lake wala kutoa ufafanuazi juu ya tukio hilo.

Juhudi za kumtafuta kamanda wa polisi mkoa ilikuthibitisha tukio hilo, ziligonga mwamba baada ya kuambiwa amesafiri kikazi wilayani Iramba, lakini ofisi yake ya habari ilidai kuwa italifuatilia tukio hilo.

No comments:

Post a Comment