Tuesday, March 18, 2014

BREAKING NEWS: WARIOBA KUWAKILISHA RASIMU YA KATIBA LEO ASUBUHI

Jaji Warioba atawasilisha rasimu ya katiba leo Jumanne kwa saa takribani nne. Ataanza saa 3.30 asubuhi hadi saa 7.30 mchana.

Baada ya vuta nikuvute ya jana bungeni, Mwenyekiti wa Bunge Maalum aliwaita wawakilishi wa makundi mbalimbali na hasa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambapo imekubalika kuwa masuala ya uendeshaji wa bunge yatafuata kanuni na taratibu.

Suala la Rais kuja kuzindua bunge la katiba siku ya ijumaa na baada ya uwasilishaji wa rasimu limeridhiwa na pande zote kwa kuzingatia kuwa hivi sasa tume ya Jaji Warioba yote ipo Dodoma na itakuwa usumbufu mkubwa iwapo watapangiwa siku ya ijumaa jioni au jumamosi baada ya ratiba ya Rais kama kanuni zinavyoelekeza.

Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka ndani ya bunge hilo, "wale watoa mada wa CCM kina Waziri Mapuri na wenzie wameondolewa. CCM walijipanga ati watoa mada wawe watu wao ili waje kufanya watakayowaelekeza, tumewakataa. Watoa mada kutoka Kenya akiwemo Amos Wako watakuja na kuseminisha."

Chanzo hicho kimesema "Tumemweleza mwenyekiti Samwel Sitta kwa uwazi kabisa, kwamba hatutakubali kuburuzwa, huu ni mchakato wa katiba, siyo bunge la bajeti la ndiyo mzee.  Katiba hii itatumiwa na vizazi na vizazi, kwa vyovyote vile lazima itengenezwe kwa misingi ya kujali utu wa kila mtu, kuheshimiana, kuridhiana na kukubaliana. Ubabe na kukiuka kanuni kwa mwanya wa Busara za mwenyekiti havikubaliki. Mwenyekiti atumie busara pale tu ambapo kanuni hazielekezi chochote."

chanzo hicho kilichukua fursa kumpongeza Mhe. Samweli Sitta kwa kujua alipoteleza na kuanguka, niendelee kumpa moyo kuwa yeye ndiye mwenyekiti wetu katika mchakato na kwamba tunamheshimu sana, lakini atambue atakapovunja taratibu au kutaka kutuburuza hatutakubali.

"Tutaendelea kuunga mkono masuala yote yenye nia njema katika mchakato huu wa katiba, lakini tutapinga kila lililo na nia ovu dhidi ya matarajio ya watanzania katika katiba."

Kikao cha maridhiano kimemalizika saa 4 usiku wa jana baada ya bunge kuahirishwa.

No comments:

Post a Comment