Jeshi la Polisi mkoani Tabora limeingia matatani baada ya kudaiwa kumpiga hadi kumuua mfanyabiashara mmoja katika soko la Kachoma, Manispaa ya Tabora, Amani Msimbe kwa kosa la kudaiwa shilingi elfu 20, 000 na mfanyabishara mwenzie.
Marehemu Msimbe alifariki dunia katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete alikolazwa baada ya kupigwa na askari akiwa kituo kikuu cha Polisi mjini Tabora.
Habari zinasema Marehemu Msimbe alikamatwa jumamosi iliyopita na kufikishwa kituo cha polisi kati kutokana na kudaiwa shilingi 20,000 na mfanyabiashara mwenzake. Baada ya kudhaminiwa na mke wake, aitwaye Anastazia Shaban alipelekwa katika hospitali ya Kitete kutibiwa majeraha aliyopata kutokana na kipigo.
Akizungumzia kifo hicho, mke wa marehemu Msimbe alisema alipompelekea chakula mume wake katika kituo cha polisi alimkuta na majeraha ambayo yalitokana na kupigwa. Alieleza kuwa baada ya kumdhamini mumewe, aliomba fomu ya polisi namba tatu yaani (PF3) ili ampeleke hospitali, lakini polisi walimnyima, wakimweleza kwamba hiyo siyo kazi yake.
Hata hivyo badaye alimpeleka hospitali ya Kitete ambako alipokelewa na kuanza kupata matibabu na yeye kutakiwa kurudi polisi kuchukua fomu hiyo ambayo bado alinyimwa na askari polisi waliokuwa zamu wakimtaka amtafute mpelelezi wa kesi hiyo ndiye ampe PF 3. Anastazia aliongeza kwamba marehemu Msimbe alikuwa na jeraha kubwa katika kiwiko cha mkono wake wa kushoto.
Kwa upande wa mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya KITETE, Dakta Deus Kitapondya, amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa chumba cha maiti kwa ajili ya kusubiri uchunguzi wa kina wa kifo hicho.
Naye Mkuu wa wilaya ya Tabora, Bw. Suleiman Kumchaya amewataka wananchi waliokusanyika nje ya lango kuu la kuingia katika hospitali hiyo wakiwa na hasira wakidai polisi wamemuua marehemu wawe watulivu wakati wakisubiri uchunguzi kamili kuhusu kifo cha mfanyabiashara huyo, Amani Msimbe.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora ACP Peter Ouma hakupatikana mara moja kuzungumzia sakata hilo baada ya simu ya kiganjani kuita na kupokelewa na msaidizi wake na kusema afande RPC yupo kwenye kikao hivyo mpigie badaye.
No comments:
Post a Comment