Friday, July 12, 2013

MISRI 'KIMENUKA' TENA



Wafuasi na wapinzani wa rais wa Misri aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi wanajiandaa kwa maandamano makubwa mjini Cairo, huku waumini wa dini ya Kiislamu wakiadhimisha Ijumaa ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadan.

Wafuasi wa Bwana Morsi wanatarajia kuwa mamilioni ya raia wa nchi hiyo, wataendelea kuunga mkono wito wao wa kutaka Bwana Morsi kurejeshwa madarakani.

Wapinzani wa rais huyo wa zamani ambao waliandamana hadi rais huyo akaondolewa madarakani na jeshi watakusanyika katika medani ya Tahrir.Watu kadhaa wameuawa kwenye ghasia zilizotokea tangu Morsi alipoondolewa.

Mwandishi wa BBC mjini Cairo, Jim Muir anasema vuguvugu la Muslim Brotherhood huenda liliwatenga raia wengi wakati wa utawala wa Morsi, lakini bado raia wengi wa nchi hiyo hawataki jeshi kuingilia masuala ya siasa.Marekani kutuma ndege za kivita Misri

Siku ya Alhamisi serikali ya Marekani, ilitoa wito kwa utawala mpya wa Misri, kusitisha harakati zake za kuwakamata wanachama wa vuguvugu la Muslim Brotherhood na kuonya dhidi ya kulenga kundi lolote.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon vile vile ameonya utawala huo wa Misri kutotenga chama chochote cha kisiasa katika harakati za kutatua mzozo wa kisiasa unaokumba taifa hilo.

Hata hivyo msemaji wa Ikulu ya White House, Jay Carney amesema, utawala wa Washington hauamini kuwa ni lazima isitishe misaada yake ya Misri.

Marekani inatarajiwa kupeleka ndege nne za vita aina ya F-16 nchini Misri, lakini haijathibitisha kuwa msaada huo utatolewa lini.

Serikali ya Marekani imesema, inachunguza ikiwa aumuzi huo wa jeshi la Misri kumuondoa madarakani rais Morsi ni mapinduzi ya Kijeshi kwa kuwa sheria za Marekani inazuia serikali kutoa misaada kwa nchi yoyote ambayo kiongozi aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia ataondolewa kupitia mapinduzi.

Wafuasi wa rais Morsi wamekuwa wakiandamana wiki nzima karibu na kambi ya kijeshi iliyoko Mashariki mwa mji mkuu wa Cairo, ambako wanaamini kuwa kiongozi wao anazuiliwa na maafisa wa kijeshi tangu alipoondolewa madarakani.

No comments:

Post a Comment