Tuesday, June 11, 2013

STARS WATUA DAR, KOCHA ALIA NA MWAMUZI


TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars, imerejea nchini jana asubuhi ikitokea Marrakesh, Morocco walikoenda kucheza mchezo wao wa Kundi C kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil mwakani.

Katika mechi hiyo iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita Morocco walishinda mabao 2-1, na hivyo kuifanya iendelee kushika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi sita ambapo Morocco wao wana pointi tano.



Timu hiyo imerejea nchini na moja kwa moja imeingia kambini katika hoteli ya Tansoma kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Ivory Coast utakaochezwa Jumapili ijayo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kocha Mkuu wa Stars Kim Poulsen alisema sasa macho yao ni katika mechi yao na Ivory Coast inayotarajiwa kuchezwa Juni 16, mwaka huu Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam.

Alisema bado uhakika wa kucheza fainali hizo za dunia upo endapo watashinda mechi zao mbili zilizosalia kwani wakicheza na Ivory Coast Jumapili, watabakiza kibarua kingine cha kucheza na Gambia ugenini.

"Pamoja na kwamba tulifungwa wachezaji wangu walicheza vizuri tatizo ni ile kadi aliyopewa Agrey Morris dakika ya 37 iliwapunguza kasi wachezaji wangu, lakini hata hivyo hawakutaka tamaa na badala yake waliendelea kushambulia na kuwawezesha kupata bao," alisema Poulsen

Alisema wana kila sababu ya kushinda mchezo ujao dhidi ya Ivory Coast, muhimu ni wachezaji wake wajitambue na wasitishwe na majina makubwa ya wapinzani wao, na pia atahakikisha anawaongezea mbinu zaidi wachezaji wake kabla ya mchezo huo.

Kwa matokeo ya mechi iliyopita  Stars inabaki na pointi zake sita baada ya kucheza mechi nne, kushinda mbili nyumbani na kufungwa mbili zote ugenini, nyingine ikiwa dhidi ya Ivory Coast.

Lakini Stars inabaki nafasi ya pili mbele ya Morocco yenye pointi tano sasa, wakati Ivory Coast wanaongoza kwa pointi zao 10 baada ya kuifunga Gambia 3-0 mechi iliyopita.

Wakati Stars ikicheza na Ivory Coast Jumapili Morocco itamenyana na Gambia.

Stars inaweza kufufua matumaini ya kucheza Kombe la Dunia ikiifunga Ivory Coast, kwani Ivory Coast ikifungwa  mechi ya mwisho na Tanzania ikashinda, itasonga mbele.

Wakati huohuo Kocha Poulsen amesema refa wa mechi yao na Morocco aliuwa mchezo kwa kutoa kadi nyekundu kwa Agrey Moris.

Akitoa maoni ya mchezo huo, Poulsen alisema alisikitishwa na jinsi refa huyo alitoa adhabu kali ambayo haiendani na kanuni za FIFA.

“Hakuwa na sababu ya kumuonesha Morris kadi nyekundu kwani tayari alishawapa Morocco penalti, alisema Poulsen huku akiongeza, “FIFA imeshawaonya marefa mara kadhaa dhidi ya kuua mchezo kwa namna hii ya kutoa adhabu kali kupita kiasi.”



No comments:

Post a Comment