Na Daudi Magesa, Majira, Mwanza
SAKATA la Meya wa Jiji la Mwanza James Bwire (Pichani Kushoto) limechukua sura mpya baada ya kunyang'anywa vitu muhimu vya utambulisho wa wadhifa wake siku chache baada ya Rais John Magufuli kuwaagiza viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kukaa mezani na kumaliza tofauti zao.
Meya huyo amenyang'anywa vitu hivyo vinavyomtambulisha kwa wadhifa wake ambavyo ni bendera ya mezani, ngao ya meya, joho na mkufu anavyovivaa wakati akiendesha vikao vya baraza la madiwani na mapokezi ya viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa.
Uchunguzi wa Majira umebaini kinachochochea mgogoro huo ni barua iliyoandikwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana Clemence Mkonda kwenda kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Mary Tesha Oktoba 25 mwaka huu akimuagiza amuandikie Mkurugenzi wa Jiji aendelee kuitisha vikao vya kikanuni na viendeshwe na Naibu Meya Bhiku Kotecha.
Tesha alitekeleza maagizo ya barua hiyo Oktoba 27 mwaka huu kwa kumuandikia barua mkurugenzi wa jiji kuendelea kufanya vikao vya kikanuni chini ya Naibu Meya Kotecha.
Siku hiyo Mkurugenzi wa Jiji hilo alimuandikia barua Meya akimtaarifu kuwa shughuli za kikanuni za halmashauri zitaendelea chini ya usimamizi wa Naibu Meya wa Jiji na Meya (Bwire) atashiriki kama mjumbe wa kawaida (Diwani).
Pia kwenye ukumbi wa mikutano na vikao vya baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kiti kinachokaliwa na Mstahiki Meya James Bwire kati ya vitatu vinavyokaliwa na Naibu Meya Bhiku Kotecha na Mkurugenzi wa Jiji Kiomoni Kibamba.
Hali hiyo imedhihirika juzi wakati wa kikao cha baraza na madiwani wa halmashauri hiyo ambacho hakikufanyika baada ya kuahirishwa na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba kinyume na kanuni za kudumu za halmashauri.
Siku chache wakati wa ujio na mapokezi ya Rais John Magufuli, meya alinyimwa gari kwa amri ya mkurugenzi na kulazimika kutumia gari lake binafsi kabla ya kukamatwa uwanja wa ndege wakati akisubiri kuungana na viongozi wengine kwenye mapokezi hayo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini vitu hivyo vimeondolewa ukiwa ni mwendelezo wa vitimbwi na mkakati wa kutaka kumng'oa kwenye nafasi hiyo unaosukwa na mkurugenzi wa jiji hilo akishirikiana na baadhi ya madiwani, wakiwemo viongozi wa serikali na chama wa wilaya ya Nyamagana.
Licha ya Rais Magufuli kuwaagiza viongozi hao wa Jiji la Mwanza kukaa mezani na kumaliza tofauti na matatizo yao agizo hilo limepuuzwa baada ya madiwani kumtii mkurugenzi na kukubali kuahirisha kikao alichokiitisha bila kufunguliwa na mwenyekiti ambaye ni meya.
kibamba hakupatika kuzingumzia suala hilo baada ya simu yake kuita bila kupokelewa huku meya akikiri kuondolewa kwa vitu hivyo ofisini na ukumbini lakini akakataa kulizungumzia suala hilo kwa undani.
No comments:
Post a Comment