Tuesday, June 25, 2013

P-FUNK PRODYUZA ALIYEWAPIKA WASANII WENGI MANGULI WA MUZIKI KIZAZI KIPYA


KATIKA fani ya muziki wa kizazi kipya nchini  hauwezi kuuzungumzia muziki huo bila ya kumtaja prodyuza mahiri Paul Matthysse  'P- Funk Majani, kutokana na juhudi zake za  kuutambulisha muziki huo kwa jamii.

P- Funk ambaye ni mmiliki wa studio ya Bongo records iliyopo jijini Dar es Salaam ameweza kuwapika wasanii wengi wa muziki huo wa kizazi kipya walio maarufu nchini
.

Mtayarishaji huyo wa muziki wa kizazi kipya miaka 22 iliyopita alionyesha hisia za kuupenda muziki na kuuendeleza nchini kutokana na hali hiyo ilimsukuma kuinua vipaji vya wasanii walio wengi ambao hadi hivi sasa wanafanya vizuri kwenye gemu hilo huku historia ikionyesha kuwa wamepitia mikononi mwa P- Funk.

Mbali na kuwa na kipaji cha kuutengeneza muziki pia aliweza kwenda masomoni ambapo alijifunza mambo mbalimbali yahusio muziki, 'Sound Engineering' kwa muda usiopungua mwaka mmoja.

Kutokana na ndoto za kutaka kuinua muziki wa kizazi kipya nchini P-Funk baada ya kusomea mambo yahusiyo muziki, mnamo mwaka 1995 aliweza kuanzisha lebo yake pamoja na kufungu studio iliyopewa jina la Bongo Records.

Akiwa bado ni prodyuza mchanga studio yake ya bongo records ilianza kupata umaarufu, kwa kipindi hicho neno la 'bongo' lilikuwa ni moja ya neno la kiswahili linalovuma na ndipo Albamu  ya Bongo Dar es Salaam ilipozinduliwa .

Kwa kipindi hiko akiwa bado ni mtayarishaji mdogo alifanikiwa kupata umaarufu mkubwa katika fani ya muziki na hasa katika mlipuko wa nyimbo za bongo fleva.

KUUTAMBULISHA MUZIKI KWA JAMII.

Mtayarishaji huyo aliweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuutambulisha muziki huo na kuufanya ukubariki kwa jamii nzima huku akipambana na ugumu wa mapokeo ya muziki huo kwenye jamii ambapo baadhi ya wazazi waliamini kuwa muziki ni uhuni.

P-Funk  aliweza kuandaa matamasha mbalimbali kwa ajili ya kutafuta vijana wenye vipaji na kuingia nao mkataba wa kufanya nao kazi katika lebo yake, alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kupata vijana wenye uwezo wa kuimba na kufanya nao kazi katika mazingira ya muziki.

Haikuwa kazi raisi kwake kuishawishi jamii kukubali kuupokea muziki wa bongo fleva kama  ni moja ya njia ya kujiajili, kutokana na kuupenda muziki na kuhitaji mafanikio ya muziki wa kizazi kipya nchini aliweza kutumia njia ya ziada ambapo jamii iliweza kuupokea  muziki huo na kuutambua kama ni njia moja wapo ya kujiajili.

P- Funk kwa kupitia  'talent shoo' aliweza kuibua vipaji vya wasanii chipukizi na vijana waliowengi kutambua vipaji vyao pamoja na kuingia katika ushindani wa vipaji walivyonavyo huku kila mmoja akiwa na kiu ya kufikia mafanikio ya kuwa mwanamuziki bora.

Kupitia Talent shoo alizozifanya na kuibua vipaji vya wasanii wachanga na baadhi ya vijana wengine kupata mafanikio ya muziki aliweza kubadili fikra za jamii na kuupokea muziki kuwa ni sehemu ya ajira na si uhuni kama hapo awali walivyofikiria.

WASANII ALIOWAINUA.

Mtayarishaji huyo kupitia mikono yake aliweza kuleta mageuzi katika tasnia hiyo ya muziki na kufanikiwa kuibua vipaji vya wasanii akiwemo Juma Nature, Solo Thang, Zay B, Sista P, Professor Jay, Lady Jaydee, ikiwa hao ni baadhi ya wasanii aliowainua kwenye maswala ya muziki.

P -Funk aliweza kumpandisha chati Juma Nature ambaye ni nyota wa muziki wa kizazi kipya, aliweza kufanikiwa zaidi alipotoa albamu yake inayojulikana kwa jina la 'Ugali' ambapo kutokana na umahili wa kushuka mistari msanii huyo iliweza kupewa vionjo na uwezo wa mtayarishaji huo kwa kutengeneza midundo yenye ujazo wa hali ya juu ambayo iliweza kufanikisha kwa kiasi kikubwa nyimbo hizo kufanya vyema katika tasnia ya muziki huo.

Mtayarishaji huyo pia ameweza kuweka rekodi ya kipekee katika tasnia ya muziki kwa kufikisha mafanikio makubwa ya uzinduzi wa albamu hiyo ya Ugali ambapo Juma Nature aliweza kufanikiwa kufanya uzinduzi wa kipekee kwa kujaza ukumbi wa Diamond kwa kiwango kikubwa cha mashabiki hadi sasa hakuna msanii yeyote aliyeweza kufanikiwa kuipita rekodi hiyo iliyoachwa na mtayarishaji huyo.

Juma Nature ambaye hadi sasa ni nyota wa muziki wa kizazi kipya huku akiendelea kuliteka soko la muziki huo ni dhahiri kuwa bila uwepo wa prodyuza huyo asingeweza kufahamika msanii huyo, P- Funk ananafasi ya kipekee kwa kuinua vipaji pamoja na kuendeleza muziki wa kizazi kipya.

Mbali na Juma Nature, aliweza kumtambulisha kwenye gemu marehemu Albert Mangwea 'Ngwair', ambaye kutokana na umahili wake wa kutambua vipaji na kutengeneza beat aliweza kufanikisha malengo ya msanii huyo na kutambulika vyema kwenye gemu hilo la muziki.

Ngwair ambaye hakufahamu kama angeweza kupata bahati ya kuingia studio na kurekodi nyimbo ikaweza kusikilizwa P-Funk aliweza kutimiza ndoto za msanii huyo na kumuibua kama msanii bora wa Hip Hop nchini.

Albamu ya 'A.k.a Mimi' ni albamu bora ya hip hop ambayo ilipikwa mikononi mwa mtayarishaji huyo huku albamu hiyo ikimtambulisha na kumuongezea mashabiki lukuki msanii huyo kwenye gemu la muziki, huku nyimbo kama 'geto langu' bado inaendelea kufanya vizuri kwenye gemu hilo.

Bado mtayarishaji huyo jina lake linaendelea kukumbukwa kwa kipindi chote cha muziki wa bongo fleva  kwa kuwapika wasanii wengine wengi akiwemo Jaydee, Zay B, Solo Thang, Professor Jay, Jaymoe na wengine wengi bila ya kumsahau Afande Sele.

Nyimbo kama Chemsha bongo, Ugali, Mkuki moyoni, Geto langu, Mvua na Jua, Maisha ya boding hizo ni baadhi ya nyimbo ambazo zilizidi kumpa mashabiki na kila mmoja kumfwatiria mtayarishaji huyo kutokana na umahili wake katika utengenezaji wa muziki.

P funk bado anandoto ya kuendelea kufanya muziki huo kuwa na mtazamo tofauti zaidi hivyo anazidi kujipanga na kuweka mikakati iliyothabiti kwa ajili ya kupambana na changamoto mbalimbali.

Akizungumza na mwandishi wa makala hii P Funk aliweka wazi kuwa sasa anajipanga kuufanya muziki kibiashara zaidi na tofauti na hapo awali ambapo aliweza kuwanufaisha wasanii wengi kupata majina na wadau mbalimbali wa muziki kufaidika kupitia kitu alichokitengeneza.

"Muziki sasa uwe na mtazamo wa tofauti inabidi tufanye muziki wa biashara zaidi sitaki kuwanufaisha watu lazima ifike hatua kila mtu apate faida kwa kile alichokifanya na siyo kunufaishana na wengine wakose mafanikio" alisema P- Funk.

Mtayarishaji huyo ambaye anaamini kipaji chake na uwezo wake aliyonao kutengeneza muziki anaamini bado ananafasi kubwa ya kuubadilisha muziki huo na kuleta muziki ambao baadhi ya mashabiki wengi wameikosa ladha hiyo.

P Funk anajipanga kuja na njia ya tofauti ya msanii kutengeneza hela na siyo kutegemea zaidi shoo kama ilivyozoeleka hivi sasa, kuwa msanii ili aweze kupata kipato chake atatumia zaidi shoo kuliko kufanya kito cha tofauti.

P Funk bado baadhi ya wasanii walio wengi wanakiu ya kufanya naye kazi huku baadhi yao wameweka wazi kuwa mtayarishaji huyo mbali na ukongwe wake wa kutengeneza muziki huo bado anajua nini anachokifanaya na kufahamu kipaji cha mwanamuziki kila anayeingia katika lebo yake.

P Funk ameweza pia kupata heshima ya muziki huo kwa kupata tuzo mbalimbali ikiwemo tuzo ya Tanzania Kilimanjaro Music Awards mwaka 2003, 2005, 2006 kama mtayarishaji bora wa muziki wa kizazi kipya, kutokana na heshima ambayo ameiweka katika tasnia hiyo bado baadhi ya taasisi zinatoa heshima kwa kumtunuku tuzo mtayarishaji huyo.

P Funk bado anahitajika kwenye gemu la muziki wa kizazi kipya kwa kuwa ni mtayarishaji wa kwanza kupigania maslahi ya mwanamuziki ili aweze kunufaika na kile anachokifanya, ni miongoni mwa watu aliyekuwa anahakikisha albamu ya msanii inaingia sokoni.

Kulingana na mambo kubadilika na wasanii wengi kuuza single kwenye matumizi ya miito ya simu, P Funk bado ananafasi kubwa ya kuhakikisha wasanii wananufaika kupitia mauzo hayo kutokana na ujuzi alionao katika suala hilo la kufanya muziki kibiashara.

No comments:

Post a Comment