Thursday, May 23, 2013

RAIS KIKWETE AWAKA VURUGU ZA MTWARA



‘Hatutakubali watu wavuruge nchi yetu kwa tamaa zao tu za umaarufu wa kisiasi, hili hapana, atakaye jaribu tutamchukulia hatua zinazohusika, na aliyemuongoza naye pia
hatutamuacha, hata kama ana mapembe makubwa kiasi gani, tutayakata tu’

Hayo ni maneno ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete akiongelea vurugu zinazoendelea Mtwara. Rais alielekeza lawama kwa wanasiasa akidai kuwa wao ni sehemu ya kuchochea vurugu hizo.

Katika vurugu hizo, polisi wamedai kukamata zaidi ya watu 90 jana waliohusishwa na matukio mbalimbali yanayohusisha vurugu hizo ikiwa ni pamoja na mikusanyiko katika makundi yasiyo maalumu pamoja na uharibifu wa mali.

Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara Linus Sintumwa amekanusha kuwepo kwa mtu yeyote kuuwawa katika vurugu hizo ambapo vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti vifo kutokea.

Vurugu za Mtwara zimetokana na vipeperushi vyenye ujumbe uliosambazwa siku za karibuni na watu wasiojulikana ukiwataka wananchi wa Mtwara kubaki nyumbani kusikiliza bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini iliyosomwa jana na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Mhongo.

Hatma ya mgogoro huo itajulikana leo baada ya kamati ya uongozi ya bunge kuwakilisha mapendekezo yake kama ilivyo agizwa na Spika Anne Makinda hapo jana ambapo shughuli za Bunge zililazimika kusimama.

Mtwara ni moja wapo ya mikoa masikini zaidi nchi Tanzania, ambapo hakuna viwanda vikubwa mkoani humo vyenye kutoa ajira. Wanamtwara wanaolala mika walikuwa na ndoto ya kuona gesi hiyo inabaki mkoani humo ili kuanzisha miradi itakayo wakomboa kiuchumi na kijamii.


No comments:

Post a Comment