Friday, May 31, 2013
MWILI WA NGWAIR KUWASILI KESHO NCHINI
MAMIA ya watanzania wanatarajia kuupokea mwili wa msanii wa muziki wa bongo fleva nchini Albert Mangwea 'Ngwair' kesho katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ukitokea Afrika Kusini.
Ngwair ambaye alikutwa na umauti nchini Afrika Kusini alipoenda kwa ajili ya shughuri za kimuziki mwili wake utawasili kesho mchana na kupelekwa moja kwa moja hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo utaagwa siku ya Jumapili katika viwanja vya Leaders Club na kuzikwa siku Jumatatu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam kaka wa marehemu Kenneth Mangwea alisema kutokana na kushindwa kukamilisha taratibu za haraka kwenda nchini humo ili kushughurikia kibali cha kuusafirisha mwili wa marehemu wametoa kibali kwa mtangazaji wa kituo cha clouds Millardayo kusimamia mwili wa marehemu kwa niaba ya familia.
Alisema kuwa Millardayo ambaye yupo nchini humo ndiye wanayemtumia kwa ajili ya kupokea taarifa zote za huko na majibu ya chanzo cha kifo cha msanii huyo yeye ndiye atakayepokea kwa niaba ya familia, kaka huyo aliwashukuru Clouds Media Group kwa kutoa mchangao wao kwa kuusafirisha mwili wa marehemu.
Kwa upande wake mtayarishaji wa muziki wa bongo fleva nchini Pfunk Majani alisema kuwa wanatafuta kila njia ili wafanikiwe kumpumzisha msanii mwenzao.
Alisema anawaomba watanzania wajitokeze kwa wingi huku kila mmoja akitoa mchangowake kwa namna mmoja au nyingine kwa kushirikiana pamoja ndio watafanikiwa.
Wakati huo kwa taarifa zilizopatikana zilieleza kuwa serikali ya Tanzania haijachangia mchango wa fedha kama inavyosemekana na badala yake imesaidia Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kupata kibali cha kusafirisha mwili wa marehemu kwa haraka.
Taarifa hizo zinasema kuwa Clouds Media Group ndio wamejitolea kuusafirisha mwili wa marehemu, na kampuni ya Push Mobile ambayo imechangia milioni tano, na kampuni ya Bongo Records imechangia shilingi milioni tano.
Kamati ya mazishi imetoa wito kwa wizara husika kujitokeza kwa ajili ya kusaidia kufanikisha mazishi ya msanii huyo Ngwair.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment