Monday, June 25, 2012

NDESAMBURO:SIASA ZA UDINI CCM ZITAIGAWA NCHI

Na mwandishi wetu

Mbunge wa Moshi Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Philemon Ndesamburo, amesema misingi mibovu ya siasa za udini iliyowekwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), itaigawa nchi na kuleta machafuko.

Bw. Ndesamburo aliyasema hayo Dar es Salaam juzi katika mkutano wa kampeni ya “Ondoa CCM Dar es Salaam”, uliofanyika Tabata Kimanga.

Alisema siasa zinazotumiwa na CCM ili kuvigawa CHADEMA na Chama cha Wananchi (CUF), zitachangia kuligawa Taifa na kusababisha machafuko ya wenyewe kwa wenyewe.

“CCM walikuwa wakisema CUF ni cha Waislamu lakini leo hii wamenda Serikali ya pamoja, hivi sasa wamegeuka upande wa CHADEMA na kusema ni chama cha Wakristo, kwa mtazamo huu chama tawala hakiwafai Watanzania,” alisema Bw. Ndesamburo.

Aliwataka vijana na wazee, kuiunga mkono CHADEMA ili iweze kuwaletea maendeleo na kuwaondoa mafisadi wanaokula fedha za umma.

Diwani wa Kata ya Kimanga, Bi. Hellen Ryatura, alisema lengo la mkutano huo kutoa elimu kwa wanachama ili waweze kufahamu misingi ya chama hicho na kuifanyia kazi kwa vitendo.

Alisema chama hicho kikichukua nchi, kitatimiza ndoto ya Watanzania ya kuwa na maisha bora kupitia misingi imara waliyonayo isiyoweza kutekelezwa na chama kingine.





No comments:

Post a Comment