Friday, May 25, 2018

MAKAO MAKUU HALMASHAURI YA BUMBULIKUJENGWA KWEHANGALA


PICHANI: Ramani ya jengo la Halmashauri ya Bumbuli litakavyokuwa. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).

Na Yusuph Mussa, Bumbuli
Immamatukio Blog

HATIMAYE Jengo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Bumbuli katika Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ujenzi wake unatarajiwa kuanza mapema Juni, mwaka huu kwenye Kijiji cha Kwehangala katika kata ya Dule B.

Hafla ya utiaji saini kwa ajili ya ujenzi huo umefanyika leo Mei 25, 2018 Ofisi za Halmashauri mjini Bumbuli na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bumbuli Ameir Shehiza, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli Peter Nyalali, baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo, watendaji na wananchi pamoja na mkandarasi.

Nyalali alisema siku hiyo ni ya aina yake, kwani ni Mungu pekee amewezesha kufikia muafaka baada ya vikwazo vingi.

"Ni Mungu pekee aliyewezesha siku ya leo kufikia hapa na kushuhudia utiaji saini kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Bumbuli, Kwehangala. Lakini kama sio yeye (Mungu), wengine sisi tungekuwa gerezani. Mtu wa pili kumshukuru ni Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli. Yeye baada ya kubaini hali halisi, aliamua kuturudishia fedha tuendelee na ujenzi.

"Shukrani pia zimuendee Mwenyekiti wa Halmashauri, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, watendaji na wananchi kwa kusaidia jambo hili kufanikiwa" alisema Nyalali.

Awali, Shehiza alimtaka Mkurugenzi Nyalali awathibitishie maslahi ya mkandarasi anaejenga jengo hilo Kampuni ya Advent Construction Ltd ya jijini Dar es Salaam kuwa yatalindwa na kufanya kazi yake kwa wakati. Lakini pia kujua ataanza lini kazi hiyo.

Mkandasi huyo Ashotosh Jog, mbele ya hafla hiyo, aliwahakikishia wananchi wa Bumbuli kuwa kazi hiyo ataifanya ndani ya mwaka mmoja, jengo la ghorofa tatu linalojengwa kwa gharama ya sh. bilioni 2,227,735,123 litakuwa limekamilika, na ujenzi wake anatarajia kuanza mapema Juni, mwaka huu.

Utiaji saini huo umefanyika ikiwa ni baada ya mvutano mkubwa uliochelewesha ujenzi huo kwa takribani miezi mitano, na Rais Dkt. Magufuli kuamua kuondoa fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi huo na kutishia kupeleka halmashauri nyingine.

Mvutano huo ulikuwa kati ya Mbunge wa Jimbo la Bumbuli January Makamba na Madiwani wa Halmashauri ya Bumbuli. Mbunge na baadhi ya madiwani walikuwa wanataka Makao Makuu yabaki mjini Bumbuli, huku baadhi ya madiwani akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ameir Shehiza na watendaji akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Peter Nyalali, wakitaka Makao Makuu yawe Kwehangala.

Wakati Makamba na baadhi ya madiwani wakidai kujenga Makao Makuu Kwehangala ni ufujaji wa fedha kwa vile tayari yapo majengo yanatumika kama Makao Makuu ya Halmashauri ya Bumbuli, na fedha hizo zingetumika kupeleka maji, dawa na barabara nzuri kwa wananchi.

Maamuzi ya Baraza la Madiwani, waliamua ujenzi wa Makao Makuu uwe Kwehangala kwa vile ndiyo kwenye eneo kubwa linalofaa kujengwa ofisi za halmashauri na taasisi zake, tofauti na Bumbuli mjini ambapo eneo lake ni finyu, na haliwezi kuwa endelevu kwa vizazi vijavyo.

Mvutano huo uliingia hadi kwenye Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Lushoto (DCC), huku Makamba akipinga mpaka kwenye kikao hicho Makao Makuu kuwa Kwehangala, hivyo maazimio ya agenda hiyo kushindwa kupelekwa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Tanga (RCC) ili yaweze kumfikia Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Ndipo Rais Dkt. Magufuli alipoona mvutano huo, akaamua 'kunyofoa' pesa za awali za ujenzi wa ofisi hizo sh. bilioni 1.5 na kusema ngoja kwanza viongozi wa Bumbuli wamalize malumbano yao.

Lakini wiki moja baada ya kauli ya Rais Dkt. Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela, Makamba, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto January Lugangika, Mwenyekiti wa Halmashauri Shehiza na Mkurugenzi wake Nyalali, walikaa kikao cha 'Demokrasia ya Uchumi' na kukubaliana Makao Makuu yajengwe Kwehangala, ndipo Rais Dkt. Magufuli alipowarudishia fedha hizo.

Madiwani wa Halmashauri ya Bumbuli wakishuhudia utiaji saini wa ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Bumbuli yatakayojengwa Kwehangala. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bumbuli Ameir Shehiza (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli Peter Nyalali (kulia) wakitia saini mkataba wa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Bumbuli na Kampuni ya Advent Construction Ltd ya jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo Ashotosh Jog na mkewe. (Picha na Yusuph Mussa), Immamatukio Blog.


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Advent Construction Ltd ya jijini Dar es Salaam akiweka saini mkataba wa ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Bumbuli yanayojengwa Kwehangala. Hafla hiyo ya utiaji saini imefanyika Mei 25, 2018 kwenye Ofisi za Halmashauri ya Bumbuli. Kulia ni mke wake. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).Na Yusuph Mussa, Bumbuli
Immamatukio Blog



No comments:

Post a Comment