Tuesday, March 06, 2018

MNEC ATOA 500,000 KUSIDIA BWENI LILILOTEKETEA KWA MOTO KOROGWE



PICHANI: Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) kupitia Mkoa wa Tangza Mohammed Salim (RATCO) akimkabidhi Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe, Anisia Mauka sh. 500,000 kama pole kutokana na tukio la kuungua bweni la wanafunzi usiku wa kuamkia jana (Picha Zote na Yusuph Mussa, IMMAMATUKIO BLOG)


Na Yusuph Mussa, Korogwe
IMMAMATUKIO BLOG

MJUMBE wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Mkoa wa Tanga Mohamed Salim ametoa sh. 500,000 kama pole kwa uongozi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe. Ni baada ya shule hiyo kupata mkasa wa kuteketea kwa moto kwa moja ya mabweni ya shule hiyo usiku wa saa 3.15 Machi 4, 2018.

Msaada huo aliukabidhi jana Machi 5, 2018 kwa Mkuu wa Shule hiyo Anisia Mauka, mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Leonard Akwilapo ambaye nae alifika shuleni hapo kujionea kadhia hiyo.

Pamoja na msaada huo, Salim aliomba Serikali kuchunguza sababu ya kuungua mabweni, kwani tatizo hilo lipo nchi nzima. "Tunaomba hili suala lifanyiwe uchunguzi kwa vile sio Tanga tu linatokea, bali na maeneo mengine ya nchi, halafu ni mabweni tu" alisema Salim.

Naye Katibu Mkuu, Akwilapo ambaye alipongeza wadau kama hao kujitokeza hata kabla ya Serikali haijafanya hivyo, alisema Serikali itarudisha kila kila kilichopotea hapo mpaka nguo za wanafunzi. "Tunaomba mfanye tathmini ya uharibifu wa mali na miundombinu iliyotokea hapo ili sisi kama Serikali tuweze kurudishia kila kitu hapo" alisema Akwilapo.

Akisoma taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela, Katibu Tawala wa Wilaya ya Korogwe Rehema Bwasi, alisema mali nyingine zilizoteketea ni magodoro 43, ambapo kati yao 26 ni ya shule na 17 ya wanafunzi. Pia vyandarua 43, shuka 86, blanketi 43, masanduku ya bati 43, mabegi 43 na fedha taslimu za wanafunzi mmoja mmoja sh. 336,500.

"Vitu vingine vilivyoungua ni pamoja na nguo za wanafunzi, miswaki, sabuni, vikombe, sahani pamoja na vitabu vya wanafunzi na vya shule. Ila tathmini inaendelea ili kuweza kujua hasara iliyotokana na moto huo" alisema.

Bwasi alisema kutokana na kadhia hiyo, baadhi ya wanafunzi walipata mshtuko, huku wengine wakiwa na magonjwa mbalimbali kama pumu na kifua, hivyo wanafunzi 41 walipelekwa Hospitali ya Wilaya na saba Zahanati ya Majengo.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) akimpa ushauri Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Leonard Akwilapo(kushoto) juu ya kwalinda wanafunzi na majanga ya mara kwa mara ya moto hasa kwenye mabweni. (Picha Zote na Yusuph Mussa, IMMAMATUKIO BLOG)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Leonard Akwilago akizungumza na viongozi wa Wilaya na Mkoa wa Tanga(Hawapo Pichani) alipofika katika shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe, jana kujionea madhara yaliyosababishwa na moto ulioteketeza bweni la wanafunzi katika shule hiyo usiku wa kuamkia jana.(Picha Zote na Yusuph Mussa, IMMAMATUKIO BLOG)


Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini, Mary Chatanda (mwenye fulana nyeupe) na Ofisa wa Elimu wa Mkoa wa Tanga, Mayasa Hashimu( kulia kwa Mbunge) wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia(hayupo pichani) baada ya kuwasili na kujionea hali ilivyokuwa baada ya moto kuteketeza bweni la wanafunzi katika shule hiyo usiku wa kuamkia jana.(Picha Zote na Yusuph Mussa, IMMAMATUKIO BLOG)




No comments:

Post a Comment