Wednesday, March 07, 2018

MBUNGE CHATANDA APOKEA PUMP MBILI ZA MAJI MTAA WA MLIMA FUNDI

Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga Mary Chatanda (wa pili kulia) akimkabidhi pampu mbili za maji Mwenyekiti wa Kamati ya Maji Mtaa wa Mlima Fundi katika Halmashauri ya Mji Korogwe Charles Gawile (kushoto). Pampu hizo zenye thamani ya sh. milioni 1.1 zitasukuma maji kwa kutumia umeme. Kulia ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlima Fundi Charles Mzuge. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Mjini Emmanuel Challe na wa tatu kushoto ni Diwani wa Kata ya Manundu Daniel Shirima.
Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Mary Chatanda akipeana mkono na mwakilishi wa Taasisi ya Fildaus Mhandisi Saburi, ambapo taasisi hiyo imemkabidhi pampu mbili za maji kwa ajili ya Mtaa wa Mlima Fundi. Makabidhiano hayo yalifanyika Machi 6, 2018 kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Korogwe mbele ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Mjini Emmanuel Challe (wa pili kushoto) na Diwani wa Kata ya Manundu Daniel Shirima (shati la kijani). (Picha Zote na Yusuph Mussa, IMMAMATUKIO BLOG).

Na Yusuph Mussa, Korogwe
IMMAMATUKIO BLOG

MBUNGE wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga Mary Chatanda amekabidhi pampu mbili zenye thamani ya sh. milioni 1.1 kwa viongozi wa Mtaa wa Mlima Fundi, Kata ya Manundu katika Halmashauri ya Mji Korogwe ili kuwapunguzia adha ya shida ya maji.

Chatanda alikabidhi pampu hizo jana Machi 6, 2018 kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maji ya mtaa huo Charles Gawile kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mtaa wa Mlima Fundi.

Alisema wakati wanasubiri ujio wa mradi mkubwa wa maji wa Mtonga kupitia Mto Pangani, tayari aliomba pampu za maji kwa ajili ya wananchi wa mtaa huo, ambapo ombi lake kwa Taasisi ya Green Crescent Ophanage limefanikiwa baada ya mwakilishi wake Mhandisi Saburi kumkabidhi pampu hizo Machi 6, 2018.

"Niliomba pampu hizi ili kupunguza makali ya shida ya maji, na kweli, wamenikabidhi pampu hizi leo (jana), hivyo nina imani kwa kiasi kikubwa zitapunguza adha ya maji kwa moja kuwekwa Mlima Fundi na nyingine Habitat.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maji Mtaa wa wa Mlima Fundi Charles Gawile, aliwatahadharisha wananchi wa mtaa huo kuwa pampu hizo zitasukuma maji kwa kutumia umeme, hivyo wawe tayari kuchangia fedha ya maji kwa ajili ya kulipa umeme.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa huo Charles Mzuge alimueleza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Korogwe Jumanne Shauri kuwa michango ya sh. 1,000 watakayochanga kwa wananchi kwa ajili ya kulipia ankara ya umeme, hawatatoa risiti ya kielektroniki.

Shauri alisema tayari kuna mradi wa maji upo Kata ya Mtonga wa sh. milioni 500 kutoa maji Mto Pangani. Mradi huo hautanufaisha wananchi wa Kata ya Mtonga pekee, bali wataweka tenki eneo la Mlima Fundi na kuweza kuwasaidia wananchi wa Kata ya Manundu kupata huduma za maji.


No comments:

Post a Comment