Wednesday, February 28, 2018

IDADI YA WATANZANIA YAELEZWA KUONGEZEKA KWA KASI

PICHANI : Idadi kubwa la watu wakitafuta mahitaji yao katikati ya jiji la Dar es Salaam, Mtaa wa Congo, Kariakoo. Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi ambazo idadi ya watu inaongezeka kwa kasi barani Afrika. (picha kwa hisani ya Mtandao)

Abraham Nyantori-MAELEZO

Tanzania ni miongoni mwa nchi sita barani Afrika zenye ukuwaji wa kasi wa ongezeko la watu na imeelezwa kuwa miongoni mwa changamoto za ukuaji huo ni uwepo wa kiwango kikubwa cha uzazi nchini.

Katika uzinduzi na uwasilishwaji wa taarifa ya takwimu za makadirio ya idadi ya watu Tanzania kwa mwaka 2017 uliohudhuriwa na wadau mbalimbali, takwimu zinaonesha pia sehemu kubwa ya watanzania watoto wakiwa asilimia 50 ni wategemezi.

Akizindua taarifa hiyo jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amebainisha umuhimu wa utumiaji wa takwimu katika kutayarisha mipango ya maendeleo ya watu lakini akatahadharisha umuhimu wa matumizi sahihi ya takwimu rasmi.

Akitahadharisha Waziri amesema, “Natoa onyo kali. Sheria namba 9 ya mwaka 2015 inaeleza wazi kuwa ni kosa kufanya utafiti au kuchapisha matokeo ya takwimu pasipo kushirikisha Ofisi ya Taifa ya takwimu”, alieleza Dkt. Mpango na kuongeza kuwa Serikali haikatazi watu au taasisi mbalimbali kufanya tafiti kwa mahitaji ya takwimu lakini ili ziwe rasmi ni lazima mbinu za utafiti ziwe rasmi kwa idhini ya Mtakwimu wa Taifa.

Waziri amesema, “Ni hatari kutofuata taratibu na maadili ya kuandaa mipango ya maendeleo ya watu ama kutatua matatizo yao pasipo kuwa na takwimu rasmi. Iwe Tanzania au mahali popote duniani” alisisitiza.

Awali, wakati wa uwasilishi, mgeni rasmi Dkt. Mpango alielezwa kuwa utafiti huo ambao unalenga kipindi cha 2013 – 2035 unakadiria Tanzania kuwa na watu 59. 4 milioni ifikapo 2021, kadhalika makadirio ya watu nchini itafikia 77.5 milioni ifikapo 2030, ambapo ni kadirio la ongezeko la watu 1.6 milioni kila mwaka.

Kuhusu kasi ya ongezeko la idadi ya watu nchini, taarifa ya Mtakwimu imeonesha kuwa kwa wastani mwanamke wa kitanzania huzaa watoto watano katika kipindi chake cha uzazi na kuongeza kuwa wanawake wa vijijini huzaa watoto wawili zaidi ukiwalinganisha na wanawake wa mjini. Hata hivyo idadi hiyo imepungua ukilinganisha na kadirio la wastani wa watoto saba kwa takwimu za mwaka 1978.

Changamoto zingine zinazosababisha uzao huu wa kasi ni matumizi finyu ya njia za uzazi wa mpango zinazoonesha ni asilimia 32 ukilinganisha na asilimia 60 kwa nchi zilizoendelea. Kadhalika kiwango cha umaskini na ukosefu wa elimu ya uzazi hasa maeneo ya vijijini.

Nchi nyingine za Afrika zenye takwimu za ukuwaji wa kasi wa ongezeko la watu ni Nigeria, Etghiopia, Afrika ya Kusini na Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Kongo.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Jacqueline Mahon ameeleza kuwa ni muhimu kufikiria kwa kina wakati wa kubuni sera muafaka ili kupunguza mwenedo unaoonekana katika matokeo ya utafiti ili kufikia malengo ya kiuchumi na kijamii na kuongeza kuwa kudhibiti kasi ya ongezeko la idadi ya watu utatoa fursa kwa watu na Serikali kuwekeza zaidi katika maendeleo ya watu.

Utafiti huo unarejea sensa yam waka 2012 na umefanikishwa na mashirika mbalimbali yakiwemo Benki ya Dunia, Jumuiya za Umoja wa Ulaya, nchi ya Kanada, Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFDI) na UNFPA.


No comments:

Post a Comment