Friday, February 16, 2018

ASKARI MAGEREZA 11 WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA MAUAJI

Na Mwandishi Wetu
Korogwe.

ASKARI magereza 11 waliopo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wamefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Korogwe na kusomewa mashitaka wakituhumiwa kumuua mwananchi wa Kijiji cha Kerenge, Kata ya Kerenge wilayani Korogwe.

Akisoma mashitaka hayo jana Februari 15, 2018, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Korogwe Kassim Mkwawa, alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kumuua Aloyce Makala wa kijiji cha Kerenge.

Mkwawa aliwataja askari hao kuwa ni P. 5377 Inspekta Makere, A. 4921 RSM (Mkuu wa Nidhamu Mokiwa Shadrack Lugendo, A. 7367 Sajenti Mussa Mdoe Seif, B. 5919 Koplo Lazaro Stephen Nyato, B. 5486 Koplo Ramadhan Yusuph, B. 7087 WDR Robert Alfred, B. 7980 Fidirishi Cosmas Joseph, B. 7248 WDR Alphonce Revocatus, B. 8911 WDR Mbesha Naftari, B. 9747 WDR Michael Elias Michael na B. 8533 WDR Hamis Halfa Msola.


Mkwawa alisema wanatuhumiwa wote kwa pamoja wamedaiwa mnamo Januari 22, 2018 katika kijiji cha Kerenge wilayani Korogwe walimuua Makala maarufu kama Mapi. Katika kesi hiyo namba 2 P 1 ya mwaka 2018, watuhumiwa wote wamekana shitaka, lakini hawakutakiwa kujibu chochote kwa vile Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya mauaji.

Shauri hilo limepangwa kutajwa tena Februari 26, mwaka huu. Na hii ni mara ya pili kesi hiyo inasomwa, kwani mara ya kwanza ni Februari 2, 2018. Na watuhumiwa wote wamerudishwa rumande.

No comments:

Post a Comment