Tuesday, October 10, 2017

TANESCO YATEKELEZA MRADI MKUBWA, VIJIJI VINGI KUUNGANISHIWA UMEME

Na Mwandishi Wetu, Njombe

SERIKALI ya Awamu ya Tano kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO), imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa upatikanaji umeme wa uhakika katika mikoa ya Njombe na Ruvuma ili kupanua shughuli za maendeleo mijini na vijijini.

Mradi huo umefadhiriwa na Serikali ya Tanzania, TANESCO na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA). Meneja anayesimamia mradi huo, Mhandisi Didas Lyamuya(PICHANI JUU), aliyasema hayo mkoani Njombe jana wakati akizungumzia maendeleo ya mradi kwa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.

Wahariri hao wapo katika ziara ya kuangalia uwekezaji unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kupitia TANESCO katika sekta ya umeme Ili kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Mhandisi Lyamuya alisema, mradi huo umegawanyika sehemu tatu ambazo ni ujenzi wa mfumo wa kusafirisha umeme kwa umbali wa kilomita 250 na njia ya umeme wa kilovoti 220 kutoka Makambako hadi Songea.


Pia mradi unahusisha ujenzi wa vituo vitatu vya kupoozea umeme kikiwemo kituo cha kupoozea Makambako 220/132/33kV na ujenzi wa vituo viwili vipya vya kupoozea umeme katika Miji ya Madaba na Songea 220/33kV.

"Mradi huu pia utahusisha upanuzi wa kituo cha kupoozea umeme Makambako 220/132/33kV" Aliongeza kuwa, mradi huo pia utahusisha ujenzi wa mfumo wa usambazaji umeme wa kilovoti 33 na kuunganisha wateja 22,700 waliopo katika mikoa ya Njombe na Ruvuma.

"Katika Mkoa wa Njombe, umeme wa kilovoti 33 utasambazwa maeneo ya Makambako, Njombe na Ludewa, kwa Mkoa wa Ruvuma ni Mji wa Songea na vijiji vilivyopo katika Wilaya za Namyumbo, Mbinga na Madaba," alisema.

Mradi pia utahusisha ujenzi wa waya wa mawasiliano 'OPGW', mfumo wa usambazaji umeme wa kilomita 900 utakaounganisha umeme katika vijiji 120 vilivyopo Songea, Mbinga, Namtumbo, Njombe na Ludewa.

Mhandisi Lyamuya alisema njia ya usafirishaji umeme wa 220kV utakamilika Machi,2018, ujenzi wake unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya Kalpataru Power Transmission Ltd.

Ujenzi wa vituo vya kupoozea umeme 220/33kV utakamilika Septemba,2018 maeneo ya Madaba, Makambako, Songea, Mkandarasi JV Shandong Taikai Power Eng Ltd & Norico International Cooperation Ltd.

Alisema ujenzi wa njia za usambazaji umeme wa 33kV, kituo cha kupooza umeme 33/11kV pamoja na uunganishani wateja kwanza 22,700 utakuwa umekamilka Desemba, mwaka huu maeneo ya Njombe na Ruvuma ambapo Mkandarasi ni Isolux Ingenierie SA.

"Wateja 12,617 wataunganishiwa umeme katika awamu ya pili, mpango huu utakamilika Novemba, 2018...hadi sasa, wateja 79 tayari wamekamilisha taratibu za malipo ya kuunganishiwa umeme kwenye Kijiji cha Lyamkena," alisema.

Akizungumzia hatua ya usambazaji umeme wa 33kV katika mikoa hiyo, alisema Mkoa wa Njombe umetekelezwa kwa asilimia 39.5, Ruvuma asilimia 63, kazi iliyofanyika ni ubainishaji maeneo ya kupitisha laini, ubunifu wa muundo wa laini.

Kazi nyingine ni ufyekaji njia za kupitisha laini, ununuzi wa vifaa, kusimamisha nguzo za msongo wa 33kV na 400V, kusambaza nyaya pamoja na usimikaji wa transfoma. Mhandisi Lyamuya alisema kazi iliyopo sasa ni kuagiza vifaa vilivyobaki, utandikaji nyaya katika nguzo, ufungaji transfoma na wateja kuunganishiwa umeme.

"Kazi ya kuunganisha umeme kwa wateja itaanza Oktoba 16, mwaka huu, katika Kijiji cha Lyamkena, eneo la Makambako, kwa Mkoa wa Ruvuma itahusisha wateja 300," alifafanua.

Kuhusu gharama za mradi, Serikali ya Sweden imetoa msaada wa krona milioni 578, mkopo wa krona milioni 42, Serikali ya Dola za Marekani milioni 20, kati ya hizo TANESCO itachangia dola milioni saba kwa ajili ya ujenzi wa laini ya msongo wa 220kV na vituo vitatu vya kupoozea umeme.

Pia Serikali imetoa sh. bilioni 7 za fidia katika maeneo yaliyopitiwa na laini kubwa itakayohusisha nguzo 710 ambazo ujenzi wake utakamilika Januari,2018. Kwa mujibu wa Mkandarasi anayejenga nguzo hizo, Satosh Gupta, kutoka Kampuni ya KPTL, hadi sasa nguzo zilizokamilika ni 266, pia wameweka msingi wa nguzo 492.


Kazi ya ujenzi wa msingi wa kufunga mitambo kwenye eneo la upanuzi wa kituo cha kupoza umeme wa 220kV Makambako ikiendelea.




Atuokoe Mhingi (katikati) kutoka TANESCO, akimuonesha Neville Meena (kushoto) fomu iliyojazwa na mmoja wa wateja wapya walioomba kuunganishiwa umeme katika eneo la Lyamkena, Makambako Oktoka 10, 2017.

 Meneja anayesimamia mradi huo, Mhandisi Didas Lyamuya, akionesha namba katika moja ya nyumba ya mteja mpya ambaye ataunganishiwa umeme katika Kitongoji cha Lyamkena, mji wa Makambako mkoani Njombe.





No comments:

Post a Comment