Monday, September 04, 2017
SERIKALI KUANZISHA TAASISI YA TEKNOLOJIA YA UJENZI
Mkurugenzi wa Barabara toka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi John Ngowi akielezea jambo wakati wa kongamano la pili la majadiliano kuhusu uanzishwaji wa Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya EcomResearch ambayo ndio mshauri mwelekezi wa uanzishwaji wa taasisi hiyo Profesa Godwin Mjema na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala toka wizara hiyo Bw. Stephen Mushi.
Na Mawasiliano,
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inatarajia kuanzisha Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) ili kuweza kuzalisha wataalam wa ngazi ya kati wenye ubobezi katika sekta ya ujenzi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Barabara Mhandisi John Ngowi wakati wa kongamano la pili la kujadili hatua mbalimbali zilizofikiwa juu ya uanzishwaji wa Taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Ngowi amesema kuwa kuanzishwa kwa taasisi hiyo hapa nchini kutawezesha kuondoa pengo la uwiano baina ya wahandisi na kada za chini kama mafundi sanifu na mafundi mchundo ambao ndio wasimamizi wa karibu wakati kazi za ujenzi zinapotekelezwa.
“Mpango mkakati wa Wizara yetu pamoja na mambo mengine, unahusisha uimarishwaji wa sera zinazohusu ujenzi kwa kujenga mazingira wezeshi,mafunzo ya ufundi na matumizi ya teknolojia mkakati ambao utawezesha kutatua changamoto za umahiri na ubobezi inayokabili sekta ya ujenzi,” amesisitiza Mhandisi Ngowi.
Aidha, Mhandisi Ngowi ameongeza kuwa uanzishwaji wa taasisi hiyo itakuwa chachu ya kufikia azma ya serikali ya awamu ya tano katika kuelekea uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa kuongeza rasilimali watu ambao ni muhimu katika usanifu, usimamizi, ujenzi na ukarabati wa miundombinu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya EcomResearch ambayo ni mshauri wa uanzishwaji wa ICoT Profesa Godwin Mjema amesema kuwa mipango ya uanzishwaji wake umefikia hatua nzuri ambapo umeshirikisha wadau mbalimbali ili kujadili Kozi na mitaala itakayotumika kufundishia.
“Sisi kazi yetu ni kushauri na leo tumekutana na wadau kujadili hatua tuliyofikia, wadu watajadili na kukubaliana na yale tuliyoandaa, wakikubaliana na sisi tutakabidhi kwa wizara ambao ndio wamiliki na wao watawasilisha Baraza la Taifa Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa hatua za usajili,”. amesema Profesa Mjema.
Kuanzishwa kwa taasisi hii kunatokana na kuendelea kupanuka kwa pengo kati ya waandisi na kada za chini hali iliyotokana na vyuo vingi vya ufundi kupandishwa hadhi kuwa vyuo vikuu katika miaka ya 1990 bila kuanzishwa vyuo vingine vya ngazi ya kati hasa vya fani ya ujenzi.
Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano.
Mwenyekiti wa Kampuni ya EcomResearch ambayo ndio mshauri mwelekezi wa uanzishwaji wa Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT), Profesa Godwin Mjema akifafanua jambo wakati wa kongamano la pili la majadiliano kuhusu uanzishwaji wa taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mkurugenzi wa Barabara toka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi John Ngowi na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala toka wizara hiyo Bw. Stephen Mushi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Bi. Segolena Francis akifafanua jambo wakati wa kongamano la pili la majadiliano kuhusu uanzishwaji wa Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) leo Jijini Dar es Salaam.
Mtaalamu wa Utafiti kutoka Kampuni ya EcomResearch ambayo ndio mshauri mwelekezi wa uanzishwaji wa Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT),akifafanua jambo wakati wa kongamano la pili la majadiliano kuhusu uanzishwaji wa taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Barabara toka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi John Ngowi (wanne kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa sekta ya ujenzi mara baada ya kufungua kongamano la pili la majadiliano kuhusu uanzishwaji wa Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) leo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa kongamano la pili la majadiliano kuhusu uanzishwaji wa Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) wakiwa katika kikundi cha majadiliano hayo yaliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo limewashirikisha wadau wa sekta ya ujenzi kutoka sehemu mbalimbali.( Picha na Idara ya Habari MAELEZO)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment