Thursday, September 07, 2017

KIWANDA KIKUBWA CHA KUCHINJA NA KUSINDIKA NYAMA CHAZINDULIWA MOROGORO (PICHA)




Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Pensheni la LAPF (LAPF Pension Fund), Eliudi Sanga, akizungumza na wageni waalikwa (hawapo pichani) kuhusu uwekezaji mkubwa na ubia wa LAPF na Nguru Hills Ranch, wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kuchinja na kusindika nyama, Nguru Hills Ranch, kilichopo Wilaya ya Mvumero, mkoani Morogoro jana.


Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mvumero, Regina Chonjo akizungumza na wageni waalikwa(hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi katika ufunguzi rasmi wa kampuni itakayoshughulika na uchinjaji, usindikaji na usafirishaji wa nyama nchini, Nguru Hills Ranch, lilipo wilayani humo, linalotarajiwa kuanza uzalishaji hivi karibuni.


Wageni waalikwa wakisikiliza maelezo kutoka kwa mwasilishaji jana katika ukumbi wa Nguru Hills Ranch wakati wa uzinduzi uliojumuisha utiaji sahihi wa mkataba kati ya LAPF na wawekezaji katika kampuni hiyo iliyoko wilayani Mvumero, Morogoro. Kuanzishwa kwa kampuni hiyo kutatoa fursa mbalimbali zikiwemo ajira zisizopungua 500, fursa kwa wafugaji kuuza mifugo yao, masoko ya nyama ndani nan je ya nchi, nk.


Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni RAS wa mkoa huo, Cliford Tandari, kizungumza na wageni waalikwa katika hafla ya uzinduzi na utiaji saini wa mikataba ya ubia baina ya LAPF na wawekezaji katika kampuni hiyo. Kulia kwa RAS ni Mkurugenzi Mkuu wa LAPF, Eliudi Sanga, na Mbia kutoka Busara Investment LLP, Lylle Webb. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa makampuni ya Zubair Corporation ya nchini Oman, Celuseri Badrinath.

NA MWANDISHI WETU, Mvomero-Morogoro

MFUKO wa Pensheni wa LAPF umefanya uwekezaji wa Dola za kimarekani Milioni 3.90 katika kiwanda cha machinjio na usindikaji nyama cha Nguru ‘Nguru Hills Ranch Limited’ kilichoko nje kidogo ya Morogoro Wilaya ya Mvomero.

Akizunguza katika uwekaji wa saini kwenye mkataba wa uwekezaji, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa LAPF, Eliud Sanga, alisema uwekaji wa saini umefikiwa baada ya tathini ya kina iliyofanywa na mfuko huo.

Alisema mfuko umejiridhisha kuhusu usalama wa rasilimali za wanachama kwenye uwekezaji huo. “Tunatambua kuwa Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika viwanda lakini LAPF imeona fursa hii ni moja wapo ambayo inakidhi vigezo vyote vya ajenda ya uwekezaji”alisema Sanga.

Alisema LAPF imewekeza kwenye kiwanda hicho kwa ubia na kampuni ya ‘Eclipse Investments LLC’ inayotokana na kampuni tanzu ya Zubair Corporation ya Oman na kampuni ya ‘Busara Investments LLP’ na kufanya wabia kuwa watatu.

“Kiwango cha uwekezaji kilichofanywa na LAPF ni USD 3.9 Milion ambayo ni sawa na asilimia 39 ya hisa za kampuni,ambapo Eclipse Investments LLC inaa hisa asilimia 46 na Busara Investments LLP ina hisa asilimia 15”alisema Sanga.

Alisema kiwanda hicho kina ukubwa wa ekari 6,000 ambapo ekari 1,200 zimejengwa miundombinu ya malisho ya mifugo kwa kipindi kisichopungua siku 90 kwaajili ya kuwanenepesha na kuwapa ubora kabla ya kuchinjwa.

Sanga alisema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo kuchinja na kuchakata ng’ombe 300 na mbuzi 2,000 kwa siku na kusafirishwa mara moja. “Nyama itakayozalishwa kwa kiwango kikubwa itasafirishwa nje kwenye nchi za mashariki ya kati na mashariki ya mbali ambako soko ni kubwa na Oman”alisema Sanga.

Alisema kiwanda hicho kinatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja 500 na nyingine zisizo za moja kwa moja na kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa ajili ya viwanda vingine.



Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa huo, Clifford Tandari (katikati walioketi) akishuhudia utiaji sahihi kuingia rasmi ubia katika kampuni ya Nguru Hills Ranch Limited. Makubaliano hayo yalisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa LAPF, Eliudi Sanga(Kulia kwa RAS), Mwakilishi kutoka Busara Investment LLP, Lylle Webb, na Celuseri Badrinath (kushoto waliokaa) Mkurugenzi Mtendaji wa makampuni ya Zubair Corporation ilyopo nchini Oman.










 Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa huo, Clifford Tandari (katikati walioketi), akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa bodi ya Nguru Hills Ranch Limited (waliosimama nyuma) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa LAPF Eliudi Sanga(Kulia kwa RAS), Mwakilishi kutoka Busara Investment LLP, Lylle Webb, na Celuseri Badrinath (kushoto waliokaa) Mkurugenzi Mtendaji wa makampuni ya Zubair Corporation na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mvumero, Regina Chonjo


PICHA ZOTE NA IMMA MATUKIO BLOG


No comments:

Post a Comment