Thursday, June 08, 2017
INTANETI INAVYOCHOCHEA UKUAJI WA UTALII BARANI AFRIKA
Na Jumia Travel Tanzania
Afrika ni bara la pili kwa kuwa na idadi kubwa ya watu ambapo inafikia takribani bilioni 1.2 (wengi wao wakiishi mijini) na inatarajiwa kongezeka mpaka bilioni 2.5 kufikia mwaka 2050 (25% ya watu wote duniani).
Kwa mujibu wa ripoti ya utalii kwa Afrika mwaka 2017 iliyofanywa na Jumia Travel imebainisha kwamba mtu mmoja kati ya watatu ni sehemu ya watu wa daraja la kati (watu wanaofanyakazi kwenye taaluma na biashara mbalimbali pamoja na familia zao) na wanatarajiwa kuongezeka mara mbili zaidi kufikia 2050. Watu wa daraja la kati ni muhimu katika uchangiaji wa ukuaji wa utalii wa ndani na ukanda mzima tuliopo.
Miongoni mwa mambo yanayochochea maendeleo na ukuaji wa sekta mbalimbali Afrika ikiwemo utalii ni pamoja na mtandao wa intaneti.
Mpaka hivi sasa, watumiaji wa mtandao wa intaneti barani Afrika wamefikia zaidi ya milioni 300, ambayo ni sawa na 9.3% ya waafrika wote na 27.7% ya ueneaji wake. Kwa kiasi kikubwa idadi hiyo imechangiwa na kuingia na kuongezeka kwa matumizi ya simu za mkononi.
Ripoti hiyo imeendelea kufafanua kuwa mnamo mwishoni mwa mwaka 2015, 46% ya waafrika walijiunga na huduma za simu za mkononi. Na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kufikia milioni 725 kufikia mwaka 2020. Na hiyo imetokana na upatikanaji wa mtandao wa intaneti wa 4G kwa zaidi ya nusu ya nchi za kiafrika, ambapo mpaka kufikia katikati ya mwaka 2016 takribani nchi 32 zilikuwa zimekwishaunganishwa na mitandao 72 ya LTE (Long-Term Evolution).
Kutokana na maendeleo hayo ya matumizi ya intaneti, sekta ya utalii hususani huduma za hoteli na malazi kwa ujumla inanufaika kwa kiasi kikubwa. Na hii ni kutokana na wateja kuwezeshwa kufanya kila kitu wakiwa mtandaoni badala ya kutembelea moja kwa moja hotelini.
Jumia Travel kwenye ripoti yake imebainisha kwamba idadi kubwa ya wateja wanatafuta na kufanya huduma za hoteli mtandaoni kwani ni salama, haraka na uhakika zaidi. Ripoti inaonyesha kwamba wateja wengi hutafuta huduma mtandaoni kwa kutumia simu za mkononi (51%) zaidi ukilinganisha na kompyuta (49%). Vivyo hivyo pia kwenye kufanya huduma yenyewe wengi hupendelea zaidi simu za mkononi (68%) dhidi ya kompyuta (32%).
Takwimu hizo ni ishara nzuri kwamba waafrika wamekubali kuyapokea mabadiliko yaliyotokana na mtandao wa intaneti hususani kwa matumizi yenye faida kwao. Kwa hiyo ni fursa kwa wadau wa sekta ya utalii kujikita zaidi mitandaoni ili kuweza kuendana na kasi ya wateja wengi wanaohamia huko.
Ingawa bado tupo nyuma kwa kiasi fulani ukilinganisha na mabara mengine lakini hali imebadilika ukilinganisha na kipindi cha nyuma. Hivi sasa, wasafiri wengi kutokana na kurahisishiwa kila kitu mtandaoni imekuwa ni rahisi kwao kufanya huduma wakiwa mahali popote na muda wowote.
Kwa mfano, wateja wengi wanaitumia njia ya mtandao kufanya huduma zao za malazi tofauti na hapo awali ambapo ilibidi kupiga simu au kwenda moja kwa moja hotelini. Mtandaoni kuna orodha ya hoteli zote, zikiwa sehemu moja, zikionyesha mahali zilipo, bei za vyumba vyake, upatikanaji wake na pia namna ya kufanya malipo. Hivyo kumrahisishia mteja kwa kuokoa muda na gharama ambavyo vingepotea kwa kutembelea hoteli moja kwenda nyingine.
Mtandao wa intaneti si tu umewarahisishia wateja kupata huduma kwa urahisi na uhakika lakini pia hata mameneja wa hoteli na wapokea huduma. Kwa mfano, kwa sasa kuna mifumo ambayo inawawezesha kuratibu mwenendo na utaratibu wa shughuli zao mahali popote walipo na muda wowote wautakao.
Mfumo huo huwarahisishia kupokea na kuthibitisha upatikanaji wa huduma, kuwa na uhakika na idadi ya vyumba walivyonavyo, kujua idadi na aina ya wateja wanaopendelea huduma zao pamoja na kupokea maoni mbalimbali juu ya huduma wanazozitoa.
Ripoti hiyo pia imebainisha kwamba orodha ya nchi nane ambazo ueneaji wake wa mtandao wa intaneti ni mkubwa barani Afrika ni kama vile; Kenya (74%), Mauritius (63%), Shelisheli (57.6%), Morocco (57.3%), Nigeria (52%), Afrika ya Kusini (51.6%), Tunisia (50.5%) na Cape Verde (44.1%).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment