Friday, June 17, 2016

IJUE SWALA YA TARAWEHE KATIKA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI

   Leo Ramadhani 11

MAELEZO YA AWALI 
Baada ya kumaliza kumi la kwanza ambalo ni kumi la rehema, sasa tuko katika kumi la kati ambalo ni kundi la MAGHAFIRA. Waumini wengi wameendelea kushindana na kupupia katika kufanya ibada. Pamoja na hayo, wapo waumini waliojisahau katika kufanya ibada na hasa Swala ya TARAWEHE 

CHANZO CHA TARAWEHE 
Swala ya Tarawehe ni Sunna maarufu, inayoswaliwa baada ya Swala ya Isha, ‎kila siku, usiku, katika Mfungo wa Ramadhani. Na imeitwa Tarawehe, kwa ‎sababu baada ya kila rakaa nne, watu hupumzika, kidogo, kisha kuendelea. ‎Na ni Swala inayo swaliwa rakaa mbili mbili, kwa kupumzika kidogo, na ‎baada ya kukamilisha rakaaa nne, basi hupumzika kwa muda zaidi. ‎
Ni Swala ambayo, siyo tu, ameiswali Mtume mwenyewe msikitini, ‎bali ameiswalisha jamaa, kwa muda wa siku tatu mfululizo. Na watu ‎walikuwa wakiongezeka kuja kuswali nyuma yake, kiasi kwamba siku ya ‎nne, msikiti haukutosha! Mtume hakutoka tena kwenda kuswali Swala ‎hiyo, licha ya watu kunadi kuwa wakati wa Swala hiyo umewadia. Mtume ‎‎hakuitikia wito wao huo. Na hakuenda msikitini, hadi alfajiri kwa ajili ya ‎Swala ya Alfajiri. ‎


Aliwaswalisha Alfajiri, kama kawaida. Lakini, alipomaliza, tu, ‎aliwageukia waumini na kuwaeleza kwanini hakuenda msikitini; alichelea ‎kwamba lau angeliendelea hivyo hivyo, na watu wakawa wanaongezeka kila ‎siku, basi ingeliwezekana ً      ikafaradhishwa Swala hiyo, juu yao. Na ‎wasingeliweza kutimiza jukumu hilo zito. Hivyo, akaonelea bora aswali ‎nyumbani, na hivyo Swala ya Tarawehe isalie kuwa ni Sunna kubwa sana, ‎katika Mfungo wa Ramadhani. Na alikuwa akiwahimiza sana watu kuiswali pasi na kuwalazimisha.

‎Imepokewa kutoka kwa Bi. Aisha ‎akisema: ‎‎“Alitoka, Mtume ‎ usiku mmoja akaenda kuswali msikitini. Watu ‎wakamfuata nyuma katika Swala yake hiyo.  Kulipokucha, watu wakawa ‎wanaambizana kuhusu swala hiyo. Hivyo, watu wengi zaidi wakajumuika, ‎siku ya pili. ‎

Mtume ‎akaenda tena usiku wa pili msikitini. Watu wengi zaidi ‎wakamfuata katika swala yake hiyo. Kulipokucha, watu wakaanza ‎kuambizana kuhusu swala hiyo. Hivyo, watu wakajumuika kwa wingi zaidi ‎msikitini.‎

Mtume akaenda tena usiku wa siku ya tatu, ambako kulikuwa na ‎watu wengi zaidi. Akaswali siku ya tatu, na watu wakamfuata kwa swala ‎yake hiyo. ‎

Ulipoingia usiku wa siku ya nne, msikiti haukuweza kuwa na nafasi ‎ya kutosha watu wote waliokwenda. Mtume hakuenda msikitini. Watu ‎wakaanza kuita kwa kusema: “Swalaaa! Swalaaa!”  Lakini Mtume ‎hajaenda! ‎

Ilipoingia Alfajiri ndiyo akaenda msikitini kwa Swala ya Alfajiri. ‎

Alipomaliza kuswali Alfajiri, aliwageukia watu na kutoa Shahada, na ‎kisha kusema: ‎" Si kama nilikuwa sijui kuhusu kujumuika kwenu jana usiku, ‎msikitini! Nilikuwa najua vilivyo!  Ila nilichelea isije Swala hiyo ‎ikafaradhishwa juu yenu, na halafu mkashindwa kuitekeleza" (Bukhari na Muslim). ‎

Inasemekana Swala hiyo ilikuwa ‎katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.” Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayra akisema: ‎Amesema Mtume ‎“Atayefanya Ibada usiku wa mwezi (mzima) wa Ramadhani, kwa Imani safi ‎kabisa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu huku akiwa na matarajio ya malipo ya ‎Mwenyezi Mungu Pekee, atafutiwa madhambi yake yote yaliyotangulia” ‎Muttafaq ‘alayhi.‎ Pia Imepokewa, kutoka kwa Abu Hurayra ‎‎akisema: “Alikuwa Mtume akiwahimiza sana watu kufanya ‎ibada usiku wa mwezi wa Ramadhani (mzima) pasi na kuwalazimisha, kwa ‎kusema: ‎‎“Atayefanya ibada usiku wa mwezi (mzima) wa Ramadhani, kwa Imani safi ‎kabisa kwa Mwenyezi Mungu, huku akiwa na matarajio ya malipo ya ‎Mwenyezi Mungu, Pekee, atafutiwa madhambi yake yote yaliyotangulia”  ‎(Muslim)

UMUHIMU WA SWALA HII
Kutokana na maelezo hayo hapo juu, Swala ya Tarawehe ni Sunna kubwa sana, na ina fadhila ‎kubwa sana, na Mtume ameiswali, na kuswalisha msikitini. Na baada ya ‎kuacha kwenda kuiswalisha msikitini, watu waliendelea kuiswali katika ‎jamaa ndogo ndogo, au kila mtu peke yake.‎

Imam Bukhari amepokea Hadithi kutoka kwa Ibn Shihab, kuhusu ‎watu kuendelea kuswali Tarawehe, katika jamaa ndogo ndogo, au mtu ‎binafsi, akisema: ‎

‎“Na mtindo huo ukaendela baada ya kifo cha Mtume na enzi ya Abu ‎Bakr na kipindi cha mwanzo cha enzi ya Umar bin al-Khattab Lakini, Umar akaona ni vyema kuwakusanya watu wote, nyuma ‎ya Imamu mmoja. Hivyo, akamtaka Ubayy bin Ka’b  aswalishe jamaa moja. 

Imepokewa kutoka kwa Abdurrahman bin Abdulqaari’ akisema: ‎‎“Nilifuatana usiku mmoja wa Ramadhani, na Umar bin al-Khattwab ‎kwenda msikitini. Akaona watu wanaswali, kwa mitindo tofauti tofauti; ‎ama wanaswali kila mmoja peke yake, au wengine wanamfuata imamu ‎mmoja, na wengine wanamfuata imamu mwengine. Basi akasema: “Ya leti ‎watu hawa wangekusanyika nyuma ya mtu mmoja. Ingelikuwa bora zaidi!” ‎Hivyo, baada ya hapo akaazimia kuwakusanya waswali nyuma ya Ubayy ‎bin Ka’b ‎(Bukhari)


MAMBO YA KUZINGATIA
Ili Muislami apate faida katika ibada hii ambayo pia hupatikana ndani ya mwezi huu, na kwa utukufu wa mwezi huu hapaswi kupuuza pia azingatie kuwa:-

‎• Swala ya Tarawehe, au Swalat al-Layl, katika Ramadhani, ni Sunna ‎Muakkadah –iliyotiliwa nguvu.‎
‎• Mtume ameswali na kuswalisha Tarawehe, msikitini, kwa muda wa ‎siku tatu mfululizo. Na kuiswali, peke yake nyumbani.‎
‎• Mtume amehimiza Waislamu –pasi na kuwalazimisha- kuswali ‎Tarawehe!‎
‎• Swala ya Tarawehe inaweza kuswaliwa bila ya jamaa, au jamaa zaidi ‎ya moja.‎
‎• Swala ya Tarawehe inaweza kuswaliwa nyumbani au msikitini.‎
‎• Wakati wa Swala ya Tarawehe ni baina ya kumaliza Swala ya Isha, ‎hadi kuchomoza alfajiri ya mwanzo.‎
‎• Kuswali Tarawehe, mara tu baada ya kumaliza Swala ya Isha na ‎Sunna zake, ndio bora zaidi, kwa wanaotaka kuswali jamaa.‎
‎• Kuswali jamaa moja, nyuma ya Imamu mmoja ni Sunna kutoka kwa ‎Mtume na vile vile, ni Sunna aliyeiendeleza, rasmi, Sayyidina ‎Umar nyuma ya Sayyidina Umab bin Ka’b!‎
‎• Kuswali jamaa moja, katika msikiti mmoja, nyuma ya Imam ‎aliyehifadhi Qur’ani, ni Sunna ilyorithiwa kutoka kwa Sayyidina ‎Umar 
‎• Ubayy bin Ka’b alikuwa haafidh wa Qur’ani, na msomaji mzuri ‎zaidi, kwa sauti, naghama na kanuni, kuliko maswahaba wengine wote. ‎Mtume‎ amesema: “Ubayy ndiye msomaji mzuri zaidi miongoni ‎mwenu!”‎
‎• Imamu bora wa kuongoza Swala ya Tarawehe ni aliyehifadhi ‎Qur’ani, na mwenye sauti nzuri. ‎
‎•‎ Mwenye kusimama kufanya Ibada Usiku wa Ramadhani, kwa ‎nia safi, na kutaraji Fadhila za Mwenyezi Mungu tu hufutiwa ‎madhambi yake yaliyopita.‎

‎• Mwenye kufanya Ibada Usiku wa Ramadhani, kwa kujionesha, ‎au kuonesha wengine kuwa yeye ni “Mwislamu” safi, hana ‎anachokipata kutoka kwa Mwnyezi Mungu.‎


No comments:

Post a Comment