Monday, February 22, 2016

MAKAMU WA RAIS : SERIKALI ITAWAPA USHIRIKIANO WAWEKEZAJI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wawekezaji kutoka China kuwa serikali itawapa ushirikiano katika kutekeleza miradi ya maendeleo watakayowekeza nchini.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo leo alipokutana na ujumbe wa kampuni ya Gezhouba kutoka China Ofisini kwake Ikulu.

Kampuni ya Gezhouba (Gezhouba Group Co. Ltd) ni kampuni ya serikali ya China ambayo ndiyo imejenga mtambo wa maji mkubwa wa kuzalisha umeme duniani unaoitwa Three Gorges ulioko China ambao una uwezo wa kuzalisha umeme wa megawatts 22,400
Kampuni hiyo imeelezea nia yake ya kutaka kuwekeza nchini katika sekta za nishati, gesi, miundombinu na kilimo cha umwagiliaji. 

Aidha kampuni hiyo imekuja kuangalia jinsi gani wanaweza kufanikisha miradi mingine kwa faida ya wananchi ikiwemo mradi wa maji Kimbiji kwa mkoa wa Dar es salaam ambapo ukifanikiwa watu zaidi ya 200,000 watafaidika na mradi huo.

“Nilipokuwa kwenye ule mkutano wa China-Afrika kule Afrika Kusini nilikutana na ujumbe kutoka China na tulizungumzia kuhusu ujenzi wa mtambo wa maji wa kuzalisha umeme,” Alisema Samia na kuongeza “Serikali ya China ni rafiki mkubwa wa Tanzania. Tunawashukuru kwa misaada mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu.”

Makamu wa Rais aliuambia ujumbe huo kuwa atazungumza na sekta husika kuona maeneo ya kipaumbele ili nayo yaweze kuingizwa kwenye orodha ya miradi ya FOCAC ili iwe rahisi kwao kwa ajili ya utekelezaji.

Katika Mkutano wa China- Africa maarufu kama FOCAC uliofanyika Afrika Kusini mwezi Disemba mwaka jana Rais wa China Xi Jinping aliahidi kutoa Dola za Kimarekani bilioni 60 kwa ajili ya kusaidia Afrika katika miradi mbalimbali ikiwemo ya nishati na miundombinu.

Wakati huo huo Makamu wa Rais alikutana pia na Mwenyekiti wa Shell Deepwater Tanzania BV Axel Knospe.
Imetolewa na 
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es Salaam
22/2/2016


No comments:

Post a Comment