Sunday, May 01, 2016

WAHALIFU WAWEKEWA MKAKATI MZITO DODOMA

Na. Frank Geofray
Jeshi la Polisi, Dodoma

Katika kuhakikisha wahalifu hawapati nafasi ya kutamba nchini, makamanda wa Polisi wa mikoa, wakuu wa upelelezi na waendesha mashtaka wameazimia kuboresha ushirikiano wao katika kufanikisha kesi za wahalifu pindi zinapofikishwa mahakamani ili waweze kupewa adhabu kali kwa mujibu wa sheria.

Hayo yamo katika maazimio ya watendaji hao wa haki jinai nchini katika kikao kazi cha siku mbili kilichofanyika mkoani Dodoma na kuwashirikisha makamanda wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa mikoa na wakuu wa upelelezi wa mikoa.

Kikao hicho kilikuwa chini ya uenyekiti wake Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu pia kilihudhuliwa na mkurugenzi wa Mashtaka nchini, DPP Biswalo Mganga, Makamishina wa Polisi, pamoja na taasisi mbalimbali zinazohusika na upelelezi na uendeshaji wa mashtaka.

Wapelelezi hao na waendesha mashtka walisema wataendeleza program za mafunzo ya pamoja katika ngazi ya mkoa, kufanya vikao vya mara kwa mara ili kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano lengo likiwa kuharakisha upelelezi na kutoa haki kwa watuhumiwa.

Aidha, wajumbe hao wa haki jinai wameazimia pia kukabiliana na changamoto ya ucheleweshaji wa upelelezi wa kesi ambapo wamekubaliana kwa pamoja kuzifikisha mahakamani kesi zote zenye ushahidi wa moja kwa moja ili kuondokana na kesi kuchua muda mrefu na kuleta malalamiko kwa wananchi.


No comments:

Post a Comment