Monday, May 02, 2016

SERIKALI KUTUMIA DOLA MILIONI 690 KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA BANDARI YA DAR ES SALAAM

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Injinia Alois Matei akiwaeleza waandishi habari kuhusu mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam utakaogharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 690 ambapo mradi huo unafadhiliwa na Serikali, Benki ya Dunia,Trade Mark East Afrika na DFID, kulia ni Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa Mamlaka hiyo Bw. Focus Mauki na mwisho Kapteni Abdullah Mwingamno wa TPA Bandari ya Dar es Salaam.
Mhandisi Mkuu wa TPA Bi Mary Mhayaya akitoa ufafanuzi kuhusu mradi wa Flow meter mpya ya Kigamboni ambao umeshakamilika na hivyo kuwezesha mafuta yote yanayoingia nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam kupimwa na kujulikana kiasi halisi kilichoingizwa hapa nchini ili kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki ikiwemo kodi .

Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na vyombo vya Habari leo jijini Dar es Salaam ukilenga kueleza mikakati ya kuboresha miundombinu ya Bandari hiyo ili kuongeza uwezo wa kupokea mizigo hadi kufikia tani milioni 38 ifikapo mwaka 2030.(Picha na Frank Mvungi-MAELEZO)

Jovina Bujulu -Maelezo

Serikali imepanga kutumia dola milioni 690 kuimarisha miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza uwezo wa kupokea mizigo hadi kufikia tani milioni 38 ifikapo 2030 kutoka tani milioni 16 za mwaka 2014/15.

Akifafanua kuhusu utekelezaji wa mradi huo wakati wa mkutano na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Injinia Alois Matei amesema mradi huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Benki ya Dunia,Trade Mark East Africa na DFID na unatarajia kuanza kabla ya mwisho wa mwaka 2016.

“ Serikali,Benki ya Dunia,Trade Mark East Africa na DFID zimetiliana saini makubaliano ya ushirikiano wa utekelezaji wa mradi wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam” alisisitiza Matei.

Akizungumazia maeneo yatakayohusika katika maboresho hayo Injinia Matei amesema kuwa yatahusisha uboreshaji na uongezaji wa kina kufikia mita 14 katika gati namba 1 hadi 7 ili kuwezesha meli kubwa zaidi kutia nanga.

Maeneo mengine ni ujenzi wa gati mpya ya kushushia magari katika eneo la Gerezani Creek, uchimbaji ili kuongeza kina cha lango la kuingilia meli hadi kufikia mita 14 pamoja na sehemu ya kugeuzia meli.

Eneo jingine ni uhamishaji wa gati la mafuta la Koj pamoja na bomba la mafuta katika eneo la ujenzi, uboreshaji wa mtandao wa reli ndani ya bandari na ujenzi wa sehemu ya kupakilia na kushushia mizigo.

Ukuaji wa kiasi cha Shehena ya mizigo inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam katika kipindi cha miaka 5 iliyopita imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 9 kila mwaka huku shehena ya mafuta na makontena ikiongezeka kwa kasi zaidi.


No comments:

Post a Comment