Thursday, May 26, 2016

TANZANIA NA CHINA KUIMARISHA MAHUSIANO

MAELEZO,

Tanzania na China kuendelea kuimarisha mahusiano katika nyanja mbalimbali zikiwemo za siasa, uchumi na utamaduni.

Ziara ya hivi karibuni ya kikazi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikinao wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima ,ikiwa ni mwaliko wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ina lengo la kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na China katika nyanja mbalimbali.

Katika ziara hiyo Dkt. Mlima pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China Bw. Zhang Ming walifanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa makampuni makubwa ya China ambayo baadhi yameshawekeza nchini na mengine yameonesha dhamira ya kuwekeza.

Aidha, Serikali ya China imesisitiza dhamira yake ya kukuza ushirikiano na Tanzania katika nyanja ya uchumi kupitia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, nishati na miundombinu. Huku kipaumbele kikiwa ni ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, pamoja na maboresho ya reli ya TAZARA na iko tayari kuanza upembuzi yakinifu wa Reli ya kati.

Kwa upande wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, kampuni ya China ya Merchant holding International (CMHI), ambayo imeingia ubia na Serikali ya Tanzania na Mfuko wa Oman kujenga bandari hiyo kwa awamu ya kwanza ambayo itakamilika mwaka huu.

Vilevile, Serikali ya China imebainisha kuwa imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu wezeshe kama barabara, nishati ya umeme, maji, na TEHAMA.

Kuhusu reli ya TAZARA Serikali ya China imesema imeridhishwa na ityahanyia kazi mazungumzo ya wataalamu yaliyofanyika jijini Dar es salaam hivi karibuni na kuahidi kuendelea kuipa kipaumbele reli hiyo kwa kuwa inabeba historia ya ya mahusiano yake na Afrika, na kutoa fedha kupitia itifaki ya 16 kwa ajili ya maboresho makubwa ya miundombinu ya reli hiyo, ikiwa ni pamoja na kushiriki kikamilifu kwenye mikutano itakayofuata inayolenga namna bora ya kuendesha reli hiyo kwa ushirikiano wa Tanzania na Zambia.


No comments:

Post a Comment