MAMLAKA ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), imeyafunga machinjio
ya Vingunguti, Dar es Salaam kwa muda usiojulikana kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo ya uchafu wa mazingira na uchakavu wa miundombinu.
Machinjiao hayo yamefungwa jana baada ya Maofisa wa TFDA kufanya
ukaguzi na kujiridhisha kuwa, mazingira yaliyopo katika machinjio hayo ni
hatarishi, si salama kwa afya za wachinjaji, wafanyabiashara na walaji wa
nyama.
Daktari Mkuu wa mifugo katika machinjio hayo, Hassan Mgwalu,
alisema TFDA wamefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha na mambo 18
yanayohusiana na mazingira, afya za walaji, wachinjaji pamoja na ubovu wa
miundombinu ikiwemo ya maji na vyoo.
Sababu nyingine ni uuzwaji nyama kuongezeka katika mazingira
hatarishi, ongezeko la idadi ya watu, uchakavu wa ndoano za kutundikia nyama,
uzio usio na ubora kiasi cha kuruhusu watu kuingia machinjioni kupitia maeneo
yasiyo rasmi.
Pia TFDA ilidai ndani ya machinjio hayo kuna idadi kubwa ya
mashimo ya kutupa nyama zisizofaa, damu kuchemshwa na kukaushwa ndani ya
machinjio, idadi ndogo ya wakaguzi wa nyama ambayo haiwiani na wanyama
wanaochinjwa.
Katibu wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Machinjio hayo, Joel
Meshack, alisema kufungwa kwa machinjio hayo ni pigo kubwa kwao kwani
hawatafanya biashara, nyama itapungua sokoni na kuwaathili walaji, wafanyakazi
katika machinjio hayo kukosa ajira.
Diwani wa Kata ya Vingunguti ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa
ya Ilala, Omary Kumbilamoto, alisema ufungwaji wa machinjio hayo utaathiri
vipato vya watu wake.
"Sehemu kubwa ya wakazi wa Vingunguti maisha yao machinjio haya, namuomba Mkurugenzi wa
Manispaa ya Ilala atekeleza kwa haraka maelekezo ya TPDF ili machinjio
yafunguliwe," alisema.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mgulumi, alisema
tayari analishughulikia kwa karibu suala hilo, taratibu za manunuzi ambazo
haziwezi kikiukwa kisheria zinaendelea, muda wowote kuanzia leo vifaa kwa ajili
ya marekebisho ya machinjio hayo vitafikishwa eneo hilo.
"Kama TFDA wameona kasoro juu ya viwango
vinavyohitajika kwa machinjio, ofisi yangu inafanya jitihada za makusudi
kurekebisha kasoro, siwezi kujua lini tutakamilisha maagizo haya,"
alisema.
Aliwatuhumu wafanyabiashara katika machinjio hayo kwa
kushindwa kufuata taratibu za uendeshaji machinjio, kuuza nyama hadi mchana
jambo ambalo halikubaliki na kuahidi kuweka utaratibu mpya machinjio hayo
yatakapofunguliwa.
Machinjio ya Vingunguti yenye wafanyabiashara zaidi ya 350
yana uwezo wa kuchinja ng'ombe 300, lakini baada ya wafanyabiashara kuongezeka
kutokana na kufungwa kwa machinjio ya Kimara, ng'ombe kati ya 550 hadi 600
wanachinjwa kwa siku.
afya ya jamii , public health ni ya muhimu kuangaliwa kwa kina na mapana
ReplyDelete