Diamond Trust Bank Tanzania, (DTB), imetangaza mafanikio makubwa
katika matokeo ya biashara kwa mwaka 2015. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa DTB
inakua kwa kasi ukilinganishwa na ukuaji katika sekta ya kibenki.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa faida kabla ya kodi mwaka 2015
ilikuwa shilingi bilioni 27.33 sawa na ongezeko la asilimia 36.03%
ikilinganishwa na shilingi bilioni 20.1 mwaka 2014.
Akiba za wateja zimekua kwa
asilimia 26.8% kutoka shilingi bilioni
570 mwaka 2014 hadi shilingi bilioni 737 mwaka 2015. Aidha, kulingana na ripoti
za mabenki zilizotolewa kwa mwaka 2015, DTB ni benki ya sita kwa ukubwa wa
amana za wateja nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa DTB, Ndg. Viju Cherian(Pichani Katikati) akizungumza na
waandandishi wa habari, alisema kuwa rasilimali za benki ziliongezeka kwa asilimia
30.5% kufikia shilingi bilioni 900 mwaka
2015 kutoka shilingi bilioni 690 mwaka 2014.
Aliongeza kuwa “Rasilimali za benki zimekuwa zikiongezeka mwaka
hadi mwaka kwa kiwango cha kati ya 26.4% na 36.4% kwa kipindi cha miaka minane
hadi mwaka 2015. Benki imeendelea kuimarika katika nyanja zote kwa kipindi hicho
huku ikiongeza mtaji wake kwa shilingi bilioni 12 mwaka 2012 na shilingi bilioni
30 mwaka 2015 kwa kuuza hisa stahiki kwa wanahisa wake.
Mikopo kwa wateja iliongezeka kwa asilimia 31.6% mwaka 2015 na
kufikia shilingi bilioni 536 kutoka shilingi
bilioni 407 mwaka 2014. DTB pia imefanikiwa kudhibiti kiwango cha mikopo isiyolipika
ndani ya asilimia 2% ikiwa ni kiwango cha chini kulinganishwa na kiwango cha
sekta ya kibenki.
Ndg. Cherian aliongeza, “DTB pia ilishiriki katika shughuli za
kijamii mwaka jana katika sekta za Afya, Elimu na Mazingira, ambapo zaidi ya
shilingi milioni 200 zilitumika. Nia na lengo kuu ikiwa ni kuboresha maisha ya
watanzania katika nyanja za elimu, afya na hata mazingiza safi na rafiki”.
DTB Tanzania ina matawi 25 nchini, ikiwa na matawi kumi na moja (11)
jijini Dar es Salaam (Mtaa wa Jamaat, Masaki, Morocco, Magomeni, Mbezi,
Mbagala, barabara ya Nyerere, Msimbazi - Kariakoo, barbara ya Nelson Mandela ,
Upanga katika barabara ya umoja wa mataifa na katika makutano ya barabara ya
Mirambo na mtaa wa Samora). Vile vile ina matawi katika miji ya Arusha (2),
Mwanza (2) na katika miji ya Dodoma, Kahama, Mbeya, Morogoro, Moshi, Mtwara,
Mwanza, Tabora , Tanga na Zanzibar.
DTB Tanzania ni mshirika wa mtandao wa maendeleo ya kiuchumi wa
Aga Khan - Aga Khan Fund for Economic Development (AKFED) ambao ni sehemu ya
mtandao wa maendeleo wa Aga Khan Development Network). DTB Kenya ni miongoni
mwa wanahisa muhimu wa DTB Tanzania.
DTB Tanzania pia ni sehemu ya mtandao wa wa mabenki ya DTB Group
yenye matawi zaidi ya 120 Afrika Mashariki katika nchi za Tanzania, Kenya,
Uganda na Burundi.
No comments:
Post a Comment