Thursday, February 25, 2016

UTAFITI: 76% YA WATANZANIA WANAAMINI ELIMU BURE NI ELIMU BORA

Asilimia 76 wanaamini kuwa elimu bure itakuwa elimu bora
Wazazi na walezi 9 kati ya 10 huchangia elimu katika shule za umma 

25 Februari 2016, Dar es Salaam: Asilimia 88 ya wananchi wote wanaamini kuwa ahadi ya elimu bure itatekelezwa katika muda uliopangwa; hii ikionesha dhahiri kuwa wananchi wana imani na ahadi hiyo. Asilimia 76 wanaamini kuwa elimu bure itakuwa elimu bora zaidi. Lakini pamoja na wananchi wengi kuwa na mtizamo chanya, asilimia 15 wanaamini elimu ya bure haitaboresha elimu. Hii ni kutokana na ongezeko kubwa la uandikishwaji wa wanafunzi ambao utatumia rasilimali nyingi.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Mwanga Mpya? Maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko kwenye sekta ya elimu. Muhtasari huu umetokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kwa njia ya simu za mkononi. Takwimu zilizokusanywa kati ya tarehe 10 Desemba, 2015 na tarehe 2 Januari 2016, kutoka kwa wahojiwa 1,894 wa Tanzania Bara (Zanzibar haimo kwenye matokeo haya).

Utoaji wa elimu bure pamoja na kukomesha michango shuleni kulikuja katika wakati muafaka. Wazazi wengi walikuwa wanaelemewa na michango ya shule. Kwa ujumla, asilimia 89 ya wazazi wanakiri kulipa michango shuleni; asilimia 80 wakiripoti kulipa mpaka TZS 50,000 kwa mwaka, huku asilimia 8 wakilipa zaidi ya TZS 100,000 kwa mwaka. Asilimia 49 wanaamini kwamba michango yao haitumiki ipasavyo na asilimia 58 wanasema michango hiyo haijaidhinishwa na serikali. Asilimia 89 wanasema walimu hutumia michango hii kujiongezea kipato.

Kwa mujibu wa wazazi, michango hutumika kulipia ulinzi (asilimia 66), majaribio (asilimia 57) na madawati (asilimia 34), huku kiwango kidogo kikielekezwa kwenye mahafali (asilimia 4), pamoja na safari za kishule (asilimia 4). Ruzuku inayopelekwa moja kwa moja shuleni ambayo ndiyo chanzo kikuu cha fedha kwa shule, inaweza isitoshe kuziba pengo la michango iliyoondolewa. Ruzuku inayotolewa huelekezwa kwenye vitabu na nyenzo nyingine za kujifunzia (asilimia 40), vifaa vya kuandikia (asilimia 20), utawala (asilimia 10), pamoja na karatasi za mitihani na uchapaji (asilimia 10).

Hivyo basi, shule zinapaswa kuwa makini na kiwango kidogo cha fedha kinachopatikana, kwani vitu vingi ambavyo wazazi huchangia havijajumuishwa kwenye ruzuku.

Pamoja na wananchi kuwa na imani na ahadi ya elimu bure, wengi wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya ubora wa elimu ya msingi kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita. Asilimia 49 ya wananchi wanasema ubora wa elimu umeongezeka, lakini asilimia 36 wanasema elimu imezorota na asilimia 14 wanasema hakuna mabadiliko yoyote.

Asilimia 37 ya wananchi wanaamini kuna uhusiano wa karibu kati ya jitihada za mwalimu na matokeo ya darasa la saba. Vilevile, wanaamini kuwa walimu ndio msingi wa maendeleo ya nchi (asilimia 93), kwamba wanaheshimika (asilimia 85), wanajivunia taaluma yao (asilimia 79), na wanapewa motisha ya kuhakikisha watoto wanajifunza (asilimia 60). Pamoja na hayo wananchi wengi wanaamini kwamba walimu hufanya kazi yao kwa ajili ya kujipatia kipato (asilimia 80).

Hata hivyo, wananchi wamekuwa na mitazamo tofauti pale walipoulizwa kama walimu wanalipwa vizuri kumudu maisha yao. (Asilimia 52 wanasema ndiyo, huku asilimia 42 wakisema hapana) na kwenye suala la mazingira ya kufundishia kama yanampa motisha mwalimu kufundisha (asilimia 58 walisema ndiyo huku asilimia 34 wakisema hapana). Wananchi wanaamini mishahara ya walimu ikiongezwa (asilimia 56) na mazingiza ya kufundishia yakiboreshwa (asilimia 19), vitaongeza ari ya walimu kufundisha.

Wananchi wameishauri serikali jinsi ya kuiboresha elimu ya msingi. Asilimia 82 wametaja masuala yanayohusiana na walimu. Wametaja ufuatiliaji wa karibu wa walimu (asilimia 40), kuongeza mishahara (asilimia 19), kuongeza idadi ya walimu (asilimia 10), kuongeza vifaa vya kufundishia (asilimia 7), mishahara kulipwa kwa wakati (asilimia 4), na kuwapatia walimu nyumba za kuishi (asilimia 2) kama suluhisho.

Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, alisema “Wananchi wameainisha kwa ufasaha changamoto zinazoikabili elimu. Ushauri na mapendekezo yao kwa serikali yamejikita kwa walimu, ikiwa ni kuwapa motisha na kuongeza uwajibikaji wao, kitu ambacho wataalamu wengi wanaafiki.”

“Lakini matumaini yao kuwa ahadi ya elimu bure itakuwa elimu bora yanaweza yasizae matunda kwa kuwa masuala muhimu ya namna ya kukabiliana na changamoto za ujifunzaji hayajaainishwa. Tumejifunza mengi katika kipindi cha miaka mingi ta utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM), ikiwemo suala la kuondoa ada na michango kutokuwa jawabu la matatizo yote. Inatia moyo kuona elimu inapewa kipaumbele cha kipekee na serikali ya awamu ya tano. Lakini hatuna budi sote kuhakikisha watoto wanajifunza wawapo shuleni. Ni wajibu wetu sote kufuatilia utekelezaji wa sera pamoja na kuwawezesha na kuwathamini walimu wetu.” alieleza zaidi.

No comments:

Post a Comment