Kampuni inayojishughulisha na uoshaji wa magari kwa njia ya
mvuke imeanza kutoa huduma zake jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mahojiano maalum Mkurugenzi Mtendaji wa
kampuni hiyo, Elia Richard Moshi alisema
kuwa lengo la kampuni hiyo ni kutoa
huduma ya kipekee kwa kuosha magari kwa kutumia mvuke ni kuzuia
uharibifu wa mazingira.
Akielezea utofauti wa huduma hiyo na huduma zingine Moshi
alisema kuwa kampuni inatumia maji yasiyo na kemikali ya aina yoyote (distilled
water) ambapo gari moja huoshwa kwa
kutumia lita tatu hadi tano za
maji kwa njia ya mvuke ijulikanayo kama steaming.
Alisema kuwa awali
alifanya utafiti na kubaini kuwa kwa kawaida gari moja huoshwa kwa kutumia lita 85 hadi 125 hali inayochochea upotevu wa
maji na uharibifu wa mazingira, hali iliyopelekea yeye kubuni
wazo la kuanzisha kampuni ya kuosha magari kwa kutumia maji kidogo
yasiyo na kemikali kwa kutumia mashine maaluum.
Aliongeza kuwa huduma nyingine wanazotoa kama kampuni ni
pamoja na kung’arisha magari kwa nje (body polishing) ili kuondoa mikwaruzo na
madoa sugu, kung’arisha gari kwa
ndani (interior polishing) na
kusafisha engine bila kutumia maji.
“Unajua unapotumia maji kuosha engine ya gari hususan kwa magari ya kisasa, unaharibu gari, hivyo
tunaosha bila kutumia maji kwa kutumia mashine maalum pamoja na kung’arisha,”alifafanua Moshi.
Aliendelea kufafanua kuwa watumiaji wa magari wanashauriwa
kuosha magari kwa kutumia mvuke angalau
mara moja kwa mwezi na kuwataka wamiliki wote waishio jijini Dar es salaam
kupeleka magari yao katika kampuni yake
yenye makazi yake katika viwanja
vya Mlimani City kwa ajili ya kuoshwa.
Akielezea malengo ya kampuni yake katika kusambaza huduma
kwa wafanyakazi waliopo maofisini, Moshi alisema kuwa kampuni ina mashine
maalum (mobile machine) zenye uwezo wa kufanya kazi sehemu yoyote ambapo wateja
wanaweza kusogezewa huduma kwenye
maofisi yao.
“Wateja waliopo maofisini wana uwezo wa kujiorodhesha na
sisi kama kampuni kuwafuata maofisini na
kuwaoshea magari yao kwenye parking zao
huku wakiendelea na shughuli zao kama kawaida na kwa usalama zaidi”
alifafanua.
Hata hivyo aliongeza kuwa kampuni ina mpango wa kufungua matawi
jijini Dar es Salaam na katika mikoa ya Arusha, Dodoma na Kilimanjaro na
mingine kwa siku za usoni
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti wakazi wa jijini Dar es
Salaam kuhusu huduma ya kampuni hiyo
walisema kuwa wameanza kunufaika na huduma hiyo na kufurahishwa na utendaji
kazi wa kampuni hiyo.
Salum Salehe mkazi wa Masaki jijini Dar es salaam alisema
kuwa tangu ameanza kutumia huduma hiyo,
gari yake imekuwa ikionekana mpya kila
kukicha na kuwataka watumiaji wengine
wa magari kutumia kampuni hiyo katika uoshaji wa magari yao.
Alisema kuwa mbali na mwonekano wa gari yake kuimarika,
kampuni hiyo imekuwa ikokoa muda mwingi kwani anakabidhi gari kwa kampuni na
kuendelea na majukumu yake kama kawaida ambapo hufuata baadaye baada ya kazi ya
uoshaji kukamilika.
Naye Victor Moshi mkazi wa Kinondoni aliongeza kuwa kampuni hiyo
imekuwa ikiwasiliana na wateja wake
kwa njia ya sms kwa ajili ya kuwashauri
juu ya utunzaji wa magari yao jambo ambalo ni jema.
No comments:
Post a Comment