Tuesday, February 09, 2016

MTANZANIA AUAWA KWENYE KASINO NAIROBI - BBC

Mtanzania huyo alitoka mkoa wa Kilimanjaro

Raia wa Tanzania ameuawa na umati mjini Nairobi baada ya kuwashambulia na kuwaua watu wawili katika kasino. Watu walioshuhudia tukio hilo wanasema mwanamume huyo alikuwa amepoteza $300 akicheza kamari.

Alijaribu kumsihi msimamizi wa kasino hiyo aruhusiwe kuweka rehani simu yake lakini akakatazwa kwa msingi kuwa haikuwa imefikisha thamani ya kuwekwa rehani, walioshuhudia wanasema.

Ni hapo ambapo anadaiwa kumdunga kisu msimamizi huyo wa kasino mtaa wa Eastleigh. Mlinzi wa msimamizi huyo alipomkabili, naye pia akamdunga kisu na kumuua. Baadaye alizidiwa nguvu na umati na kuuawa.

Ripoti zinasema mwanamume huyo alitoka mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania na alikuwa akifanya kazi kama fundi wa viatu kabla ya kuanza biashara ya uchukuzi wa kutumia pikipiki, maarufu kama bodaboda nchini Kenya. Kabla ya kisa hicho, waliokuwa wakifanya kazi naye wanasema alikuwa ameuza pikipiki hiyo.

No comments:

Post a Comment