MAELEZO.
SHIRIKA la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) limetolea ufafanuzi kuhusu malalamiko ya Wakazi wa kijiji cha Seseko Kata ya Mwamalili mkoani Shinyanga.
Ufafanuzi huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Meneja Uhusiano wa Shirika hilo, Bw. Adrian Severin wakati akiongea na Idara ya Habari mara baada ya kuhojiwa kuhusu madai ya wakazi wa kijiji hicho kuhusu kufyekwa kwa mazao yao bila ya kulipwa fidia na Shirika hilo.
Severin amefafanua kuwa madai ya wakazi wa eneo hilo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara licha ya TANESCO kuwalipa fidia kwa wakazi hao tangu mwaka 1999.
Severin amefafanua kuwa, Madai hayo yanatokana na njia ya msongo wa Umeme wa kilovoti 220 ambayo ni njia inayotokea Shinyanga kuelekea Mwanza na inaonekana hawa wanaolalamika kufyekewa mazao yao ni wale ambao wamevamia ama wameweka makazi yao hivi karibuni katika maeneo hayo kwasababu Shirika la TANESCO lilishawalipa wakazi ambao walipitiwa na nguzo hizo tangu mwaka 1999.
Aidha, Bwana Severin aliongeza kuwa, TANESCO kabla ya kupitisha nguzo katika maeneo ya makazi ama mashamba ya wananchi huwa wanawasiliana na uongozi wa eneo husika na kukubaliana na wananchi wenyewe ili waruhusiwe kupitisha ama kutopitisha nguzo za umeme, na ilipotokea wanakubaliwa basi fidia inalipwa kwa wakati na kwa kufuata utaratibu ikiwemo kufanya tathmini ya kutosha na kisha kuwalipa kwa wakati kulingana na matakwa ya Sheria.
‘’Wakati mwingine baadhi ya wananchi wamekuwa wasikivu kwa kukubali na kuruhusu kupitisha nguzo za umeme katika maeneo yao na tumekuwa tukiwalipa fidia, lakini kuna wengine wamekuwa wakifanya shughuli za kibinadamu ikiwemo ulimaji mazao chini ya laini za umeme kwa makusudi ili walipwe fidia pindi yakifyekwa, hawa wanakuwa wanavunja utaratibu ambao umewekwa na TANESCO kuwa, ndani ya mita thelathini kwa pande zote mbili ambazo laini zinapita hakutakiwi kufanyika shughuli yoyote ya makazi au maendeleo, hivyo katika ukaguzi wetu tunapofika na kukuta wamekiuka taratibu hizo tunazuia uendelezaji wa shughuli hizo na hasa kubwa likiwa ni suala la usalama wa mali na maisha yao wenyewe wananchi.’’, alisema Severin.
Amewahasa wakazi nchini kote kuzingatia Sheria ya mita 60 kwa kutofanya shughuli zozote za kibinadamu chini ya nguzo za umeme kwa ajili ya usalama wa maisha yao kwani umeme upitao unakuwa ni wa msongo mkubwa hivyo unaweza kuhatarisha maisha yao endapo wanakaidi kufanya hivyo.
‘’Napenda kusisitiza kuwa, wananchi wazingatie na kuhakikisha kuwa hawafanyi shughuli zozote za kiuchumi au ujenzi wa makazi ndani ya eneo la mita 60 kutoka kilipo chanzo cha umeme ili kuondoa kero na madai kama haya’’, alisisitiza Severin.
No comments:
Post a Comment