Monday, November 23, 2015

WAKENYA WAJIANDAA KUMPOKEA PAPA FRANCIS, ULINZI KUIMARISHWA

Serikali ya Kenya imesema maandalizi ya kumlaki Papa Francis nchini Kenya yamekamilika na ziara yake inatarajiwa kuwa ya kufana.

Kwenye kikao na wanahabari, Msemaji wa Ikulu Manoah Esipisu na Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet walisema hatua madhubuti zimechukuliwa kumpokea kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani.

“Hili ni tukio muhimu sana, nchi yetu inamkaribisha Papa Francis kwa mara ya kwanza barani Afrika, na ningependa kusema kwamba tuko tayari kumpokea pamoja na msafara wake, usalama umeimarishwa tukiangazia kuanzia kuasili kwake, njia atakazotumia na pia kwa wageni wote watakaomiminika jijini hapa,” alisema Bw Boinnet.
Barabara atakazokuwa akipitia Papa Francis zitafungwa zikiwemo Mombasa Road, Uhuru Highway, Waiyaki Way na Thika Road, hatua ambayo inatarajiwa kuathiri uchukuzi jijini.

Katika mkutano huo na wanahabari askofu Alfred Rotich anayewakilisha maaskofu wa Kikatoliki nchini Kenya, alieleza kuridhishwa kwake na maandalizi na kuwakaribisha Wakenya kushiriki misa.

Hata hivyo amesema mapadri ambao wamekiuka kanuni ya useja, hawatakaribishwa kumuona Papa Francis.

“Hili ni ombi la kanisa kwamba tuendelee na useja, sisi ni watu ambao tunatii viapo vya umaskini, watu wenye roho safi, na watiifu, kama kuna kuhani yeyote ambaye alijiondoa katika kanisa halisi la katoliki, hatutawakaribisha kamwe,” alisema.

Papa Francis atawasili Nairobi Jumatano tarehe 25 mwendo wa alasiri, na moja kwa moja ataelekea kwa ikulu ya Rais kugagua gwaride na kuhutubia taifa kwa pamoja na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Alhamisi tarehe 26, kutakuwa na mkutano wa dini nyumbani kwa mwakilishi wa Vatican nchini Kenya, halafu hapo baadaye ataelekea katika chuo kikuu cha Nairobi kuongoza misa kabla ya kuandaa kikao cha maaskofu na viongozi wa dini.

Ijumaa tarehe 27 ataelekea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi katika kitongoji cha Kangemi viungani mwa mji wa Nairobi, na baadaye kuelekea katika uwanja wa Kasarani kuhutubia vijana.
(BBC SWAHILI)


No comments:

Post a Comment