Monday, June 02, 2014

WANAWAKE WABAKWA GEREZANI

Utafiti uliofanywa na shirika moja la misaada Uingereza umeonesha kuwa ubakaji unatumiwa tena kwa kiasi kikubwa gerezani kama adhabu kwa wanawake wanaojihusisha na masuala ya siasa nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Congo.

Utafiti huo uliofanywa na "Freedom from Torture" umegundua kuwa zaidi ya nusu ya wanawake wote walio fanyiwa uchunguzi walikuwa wamebakwa na magenge.

Shirika hilo ambalo huwasaidia waathiriwa wa ubakaji umewafanyia uchunguzi wanawake 34. Ubakaji umekuwa ukitumika kwa miaka mingi kama silaha katika vita vya mashariki mwa DRC lakini shirika la ''Freedom from Torture'' linasema kuwa sasa wanawake magerezani kote nchini humo wanabakwa kama njia moja ya kuwaadhibu na kuwanyamazisha kutozungumza au kuchangia siasa za nchi hiyo.

Wanawake hao waliofanyiwa uchunguzi wanajumuisha wachuuzi, wasomi na hata wataalamu mbali mbali kati ya miaka 18 na 62 kote nchini humo.

Takriban hao wote walitiwa nguvuni kwa kujihusisha na masuala ya haki za binadamu au kampeini za kisiasa, au hata jamaa katika familia yao alihusika na siasa.

Zaidi ya nusu ya wanawake hao wanasema wamebakwa na magenge hata wanaofika kumi. Shirika hilo sasa linataka serikali ya DRC kufanya hima kutekeleza azimio la umoja wa mataifa dhidi ya kuwatesa watu.(BBC)

No comments:

Post a Comment