Timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inashuka
dimbani leo Uwanja wa Taifa wa Harare mjini hapa kumenyana na wenyeji Zimbabwe
katika mchezo wa marudiano hatua ya kwanza ya mchujo ya Fainali za Kombe la Mataifa
ya Afrika (AFCON) 2015.
Tanzania iliyoshinda 1-0 bao la John Bocco wa Azam FC katika
mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo itahitaji
sare yoyote kusonga mbele katika hatua ya mwisho ya mchujo, ambako ikifuzu itapangwa kwenye Kundi kuwania tiketi ya Morocco 2015.
Stars iliyofikia katika hoteli ya Best City Lodge mjini hapa,
pamoja na misukosuko waliyoipata juzi mjini hapa ya kufungiwa vyumba vya hoteli
kwa saa mbili, wachezaji wake wanaonekana kuwa katika morali ya hali ya juu
kuelekea mchezo huo.
Kocha Mart Nooij raia wa Uholanzi bado ni mwenye kujiamini
kuelekea mchezo huo licha ya matokeo ya ushindi mwembamba Dar es Salaam na
amesema watacheza kwa kujiamini leo. Zimbabwe imekiongezea nguvu kikosi chake kwa wachezaji
waliokosa mchezo wa kwanza ambao wanacheza soka ya kulipwa Afrika Kusini na
nchi nyingine.
Kwa ujumla, Zimbabwe imeweka nguvu nyingi katika mchezo huo
kuhakikisha inapindua matokeo na kuitoa Tanzania. Lakini Tanzania ina kumbukumbu nzuri katika mechi zake za
miaka ya karibuni nchini hapa kwa ngazi ya klabu na kimataifa.
Mwaka 2001 klabu ya Yanga baada ya sare ya 2-2 Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Highlanders katika Ligi ya Mabingwa Afrika ilifanikiwa
kuifunga timu hiyo 2-1 mjini Bulawayo na kusonga mbele.
Lakini mchezo haukumalizika baada ya Yanga kupata penalti
ikiwa inaongoza 2-1 ambayo wenyeji waliigomea na kuanzisha vurugu, zilizosababisha
mchezo kuvunjika. Yanga ilisonga mbele na kwenda kutolewa na Mamelodi Sundowns
ya Afrika Kusini.
Mwaka 2005, timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya
miaka 17 ilianza kwa ushindi wa 2-0 Dar es Salaam na katika mchezo wa marudiano
mjini Bulawayo ikashinda pia na kuitoa Zimbabwe. Hata hivyo, pamoja na Serengeti Boys kufuzu fainali za U17
Afrika zilizopigwa Gambia, lakini ilienguliwa kwa tuhuma za kumtumia Nurdin Bakari
akiwa amezidi umri, wakati huo akichezea Simba SC.
Kikosi cha Tanzania leo hakitarajiwi kuwa na mabadiliko
makubwa kutoka kile kilichocheza mechi ya kwanza na kushinda 1-0 Dar es Salaam
bao pekee la John Bocco ‘Adebayor’.
Bila shaka Nooij ataawaanzisha tena pamoja washambuliaji
watatu, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu wote wa TP Mazembe ya DRC na Bocco,
wakati katika safu ya kiungo Mwinyi Kazimoto wa Markhiya ya Qatar na Frank
Domayo wa Azam watapewa majukumu.
Mrisho Ngassa wa Yanga SC atacheza pembeni akiwa na jukumu
la kutengeneza mashambulizi na kusaidia safu ya kiungo.
Shomary Kapombe atacheza tena beki ya kulia, wakati kushoto
kuna uwezakano Erasto Nyoni, wote wa Azam FC akaanza badala ya Oscar Joshua na
mabeki wa kati bila shaka watapangwa tena Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan, wakimlinda kipa Deo Munishi ‘Dida’, wote wa
Yanga.
Bado Stars itakuwa na hazina nzuri katika benchi ya
wachezaji hodari kama Simon Msuva, Ramadhani Singano ‘Messi’, Haroun Chanongo na
wengineo. Ikumbukwe huu utakuwa mchezo wa pili wa mashindano kwa Nooij
tangu arithi mikoba ya Mdenmark Kim Poulsen baada ya wa awali na Zimbabwe Dar
es Salaam.
Aidha utakuwa mchezo wa nne kwa ujumla tangu aanze kazi
Taifa Stars akitokea St George ya Ethiopia, mechi nyingine mbili zikiwa dhidi ya
Malawi, moja akitoa sare ya bila kufungana Mbeya na nyingine akishinda 1-0 Dar
es Salaam. Mungu ibariki Tanzania, ibariki Taifa Stars. Amin
No comments:
Post a Comment