Mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania Bara, Azam Fc ndani ya
siku mbili wamefanya usajili wa wachezaji wawili kutoka klabu ya Yanga SC ikiwa
ni sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya kocha mkuu, Mcameroon, Joseph Marius
Omog.
Mapema wiki hii walifanikiwa kumsainisha aliyekuwa mshambuliaji wa
Yanga, Mrundi Didier Kavumbagu kwa mkataba wa mwaka mmoja, huku kipengele cha
kuongezewa mwaka mwingine kikiwepo kulingana na uwezo atakaouonesha.
Wakati wapenzi wa soka wakijadiliana usajili wa Kavumbagu, juzi wengi walishituliwa na usajili mwingine mkubwa wa kiungo mahiri wa ukabaji
wa Yanga, Frank Domayo `Chumvi”. Domayo alisaini Mkataba wa miaka miwili
kuitumia klabu ya Azam, huku taarifa zikieleza kuwa mkataba wake na Yanga
ulikuwa umemalizika mwishoni mwa msimu uliopita.
Usajili wa Domayo ulifanyika jana katika kambi ya timu ya
taifa ya Tanzania, Taifa Stars iliyopo Tukuyu jijini Mbeya kwa maandalizi ya
mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi mei 4 mwaka huu uwanja wa
Sokoine jijini Mbeya.
Stars ipo katika mipango ya mchezo huo na wachezaji wote
wanaufikiria, lakini kwa Domayo imekuwa tofauti ambapo akiwa huko ameamua
kusaini Azam fc. Ukirejea nyuma sio mara ya kwanza mchezaji kusaini akiwa
katika kambi ya timu ya taifa ya Tanzania. Kelvin Yondani wakati anasaini Yanga
kutokea Simba alikuwa kwenye kambi ya Taifa stars.
Ilielezwa kuwa alitoroshwa na kiungozi mmoja kwenda kusaini
Yanga. Kitendo kile kilitafsiriwa kuwa utovu wa nidhamu, lakini baadaye suala
hilo lilizimwa kiaina kwasababu ni utamaduni wetu.
Domayo si mara yake ya kwanza, kwasababu miaka miwili
iliyopita wakati akijiunga na Yanga kutoka JKT Ruvu alisaini mkataba wake akiwa
kambi ya Stars. Baada ya usajili huo kukamilika, Katibu wa Azam FC, Nassor
Idrisa Mohamed ‘Father’ amekaririwa na tovuti ya Azam akisema katika kuendelea
kukiimarisha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao wamepiga hatua nyingine kwa
kumsaini Domayo.
“Kama unavyojua, baada ya kumaliza msimu vizuri tukiwa
mabingwa wa Bara, tuligundua mapungufu kwenye kikosi chetu na kwa ushauri wa
mwalimu wetu (Joseph Marius Omog) ndiyo tunayafanyia kazi,”alisema Father.
Domayo anakuwa mchezaji wa wa pili ndani ya siku mbili
kusajiliwa na Azam FC kutoka mabingwa wa zamani na mabingwa wa kihistoria
Tanzania Bara, Yanga SC baada ya jana klabu hiyo kumsaini mshambuliaji Mrundi
Didier Kavumbangu.
Kufautai usajili wa aina hiyo kujitokeza tena katika kambi
ya Taifa stars, shirikisho la soka Tanzania, TFF limeshituka na kuanza taratibu
za kuchunguza suala hilo linaloihusisha Azam fc na mchezaji Frank Domayo akiwa
kambini.
Taarifa iliyotumwa na afisa habari wa TFF, Boniface Wambura
Mgoyo, asubuhi hii inasema kuwa: “Kutokana na tukio lililotokea jana (Aprili 30
mwaka huu) kwenye kambi ya timu ya Taifa (Taifa Stars) iliyopo Tukuyu mkoani
Mbeya likihusisha usajili wa baadhi ya timu, Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemteua Wakili Wilson Ogunde kuchunguza
mlolongo mzima wa tukio hilo.
Baada ya kukamilisha uchunguzi wake, Wakili Ogunde
ataishauri TFF kuhusu hatua za kisheria na kikanuni za kuchukua. TFF inatoa
wito kwa wachezaji, klabu na wadau wa mpira wa miguu kufuata kanuni na taratibu
katika utendaji wao”.
No comments:
Post a Comment