Friday, April 18, 2014

KESI YA TWIGA YAZIDI KUKWAMA, MSHTAKIWA KATOKOMEA KUSIKOJULIKANA

Moshi

Upande wa Jamuhuri katika kesi ya utoroshwaji wa wanyama hai zaidi ya 100 wakiwamo Twiga na ndege wa aina mbalimbali kwenda Qatary, umeieleza mahakama kwamba mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Kamran Ahmed hajapatikana.

Wakili wa jamuhuri katika kesi hiyo,Patrick Mwita aliieleza mahakama ya hakimu mkazi mjini Moshi inayosikiliza kesi hiyo chini ya hakimu, Simon Kobelo kwamba mshtakiwa huyo raia wa Pakistan hajakamatwa.

Wakili Mwita,mbele ya wakili John Lundu anayemtetea mshtakiwa wa pili, Hawa Mang'unyuka, aliieleza mahakama kwamba mshtakiwa wa kwanza hajaonekana lakini pia hakuna taarifa zozote kutoka kwa wakili wake,Edmund Ngemela ambaye naye hakufika mahakamani hapo.


"Mheshimiwa naomba hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa wa kwanza iendelee kutumika pamoja na hati ya kuuitwa kwa wadhamini wa mshtakiwa huyo itumike ili wafike mahakamani hapa'alisema.

Kutokana na taarifa hiyo, hakimu Kobelo alimhoji wakili Lundu iwapo ana taarifa zozote za wakili Ngemela ambapo alijibiwa kuwa waliwasiliana na kumweleza kuwa anauguliwa na mkewe.

Aidha hakimu Kobelo, alisema kesi hiyo itaendelea Mei 6 na 7 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali lakini akitaka mshtakiwa wa kwanza kufikishwa mahakamani hapo.

Kesi hiyo inawakabili washtakiwa wanne akiwamo raia wa Pakistani, Ahmed ipo katika kutolewa kwa ushahidi upande wa jamuhuri na tayari mashahidi 21 wameshatoa ushahidi wao.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo wametajwa kuwa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Osaka Traders, Hawa Mang'unyuka,Ofisa Mifugo wa Shamba la Wanyama, Martin Kimath na Ofisa Usalama wa Kadco, Michael Mrutu.

Washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali ya uhujumu uchumi ikiwamo la kusafirisha wanyama hai zaidi ya 100 wakiwamo Twiga wanne na ndege aina mbalimbali kwenda Doha,Qatary na kuisababishia Serikali hasara ya Sh Mil 170.5.

TAFADHALI CHANGIA MAWAZO YAKO HAPA CHINI. . .

No comments:

Post a Comment