Wednesday, February 12, 2014

JAMII YASHAURIWA KUACHA TABIA YA KUWANYANYAPAA WAJANE

Jamii imeshauriwa kuacha tabia ya kuwanyanyapaa wajane na watoto kwa kuwanyanganya mali zilizoachwa na ndugu zao pindi wanapokufa kwani kufanya hivyo ni unyanyapaa wa kijinsia.

Wito umetolewa na Dkt. Monica Mhoja Mwezeshaji wa Mafunzo yaliyohusu kuwajengea uelewa waandishi juu ya Sheria na Sera mbalimbali zilizopo zinazohusiana na masuala ya ukatili wa kijinsia hapa Nchini wakati wa Semina ya siku moja kutoka Shirika la EngenderHealth Mradi wa CHAMPION.

Alisema ni jambo la kusikitisha kuona mjane pindi mwenza wake anapokufa ndugu wanamnyanganya mali na kusema ni vyema sasa jamii ikaacha kufanya hivyo kwani ni unyanyapaa wa kijinsia.

"Jamani ndugu zangu waandishi tusaidiane katika hili...tunaomba na hao ndugu watafute mali zao na si kusubili ndugu wakifa au kutengana ndipo wachukue mali kwani kufanya hivyo ni unyanyapaa uliokithiri ambao binadamu hapaswi kuufanya,"alisema.


Aidha alisema kuwa suala la unyanyapaa ni moja ya changamoto ambayo inaikabili jamii na kutolea mfano kuwa katika nchi zingine zilizoendelea wanaofanya hivyo huwa wanawajibishwa.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki, alisema "kwanza napenda kuwajulisha kuwa kukutana kwetu leo ni kukuza uelewa wa waandishi juu ya sheria na sera mbalimbali zilizopo zinazohusiana na masuala ya ukatili wa kijinsia hapa nchini,".

Alisema pamoja na kwamba matendo hayo yanaendelea kutendeka ndani ya jamii lakini waandishi wanayo nafasi kubwa ya kuielimisha jamii na badaye vitendo hivyo vikaweza kupungua kama siyo kuisha kabisa.

"Lakini nitoe shukrani zangu kwa Mradi wa CHAMPION na shirika lake linalotoa ushauri wa kitaalamu na fedha kwani imelenga kutoa mafunzo sehemu sahihi kabisa kwani kufanya hivi kutaweka bayana athari za kijamii za sera na sheria zilizopo zinazohusiana na ukatili wa kijinsia na mapungufu yaliyopo,"alisema.



No comments:

Post a Comment