Mwenyekiti wa taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt Shukuru Kawambwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya WAMA Nakayama Dkt Ramadhani Dau na Mkuu wa Shule hiyo wakiangalaia matumizi ya ya Tabuleti 61 katika darasa la kidato cha pili katika Shule ya Wama Nakayama iliyoko kijijini Nyamisati, Rufiji, Mkoa wa Pwani leo Januari 27, 2014 toka kwa Mwenyekiti wa taasisi ya kusaidia elimu ya Opportunity Education Foundation wa Marekani Bw. Joe Ricketts akikabidhi moja ya Tabuleti 61 alizozitoa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha pili katika Shule hiyo.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali kusambaza tabuleti za kufundishia sekondari
Yaanza kazi hiyo kwa kushirikiana na taasisi ya Marekani ya Opportunity Education Trust
Serikali inakusudia kutoa maelfu kwa maelfu ya tabuleti za kufundishia masomo mbali mbali kwa wanafunzi na walimu wa shule za sekondari nchini kama njia ya ubunifu zaidi, ya kisayansi na ya uhakika ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).
Ili kufanikisha mpango huo, Serikali inakusudia kuingia ushirikiano (partnership) na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Opportunity Education Trust ya Marekani ambayo leo, Jumatatu, Januari 27, 2014, inazindua mpango wa majaribio wa utoaji wa tabuleti hizo kwa wanafunzi na walimu wao wa shule za sekondari nchini.
Mpango wa Serikali wa kusambaza tabuleti kwa wanafunzi na walimu wa shule za sekondari ulitangazwa usiku wa jana, Jumapili, Januari 26, 2013 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipokutana na kuzungumza na Bwana Joe Ricketts, mwenye taasisi ya Opportunity Education Trust na mmoja wa matajiri wa Marekani.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amemweleza kwa undani Bwana Ricketts hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali yake kupania na kuboresha elimu tokea mwaka 2006, hatua ambazo zimechangia kupanua kwa kasi na kwa kiwango kikubwa wigo wa utoaji elimu nchini na changamoto ambazo zimezuka kutokana na upanuzi huo mkubwa.
Rais Kikwete amesema baadhi ya changamoto hizi ni ukosefu wa walimu, na hasa walimu wa masomo ya sayansi, na ukosefu wa vitabu vya kufundishia changamoto mbili kubwa ambazo zinatatuliwa na matumizi ya tabuleti.
“Mbali na upanuzi mkubwa wa nafasi za wanafunzi kupata elimu ya ngazi mbali mbali, pia tumepanua sana ufundishaji wa walimu. Mwaka 2005, vyuo vyetu vyote vilikuwa vinatoa walimu 500 sasa tunatoa walimu 12,000 kwa mwaka. Hivyo, tunaamini kuwa katika mwaka mmoja ama miwili ijayo, tutakuwa tumemaliza tatizo la walimu wa masomo ya sanaa,” Rais Kikwete alimwambia Ricketts na kuongeza:
“Lakini bado tunakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi, kama zilivyo nchi nyingine. Tuna upungufu wa walimu 26,000 na kwa mwaka vyuo vyetu vyote vinahitimisha walimu 2,100 tu. Hii ina maana kuwa itabidi kusubiri miaka 13 kuweza kumaliza tatizo hili kwa mahitaji ya sasa. Hili haliwezekani na hii ndiyo maana halisi ya kutumia sayansi na teknolojia ya namna hii kufundishia wanafunzi wetu.”
Rais Kikwete alisema kuwa matumizi ya teknolojia kufundishia nchini ni jambo linalowezekana kwa urahisi kwa sababu mtandao wa mawasiliano wa National Fibre Network ambao karibu umefikia kila wilaya sasa.
Rais Kikwete alimshukuru Bwana Ricketts na taasisi yake kwa kukubali kuchangia maendeleo ya sekta ya elimu nchini kwa kusambaza teknolojia ya kisasa kama moja ya njia za ubunifu zaidi za kufundishia hasa masomo ya sayansi.
Chini ya mpango huo wa majaribio wa kusambaza teknolojia hiyo ya kisasa, taasisi ya Opportunity Education Trust inatoa tabuleti 1100 kwa ajili ya walimu na wanafunzi wa sekondari katika shule 33.
Bwana Ricketts ambaye ni mwenyeji wa Omaha, Nebraska alimwambia Rais Kikwete: “Hapa tunafanya majaribio na Tanzania ni nchi ya kwanza duniani miongoni mwa nchi ambazo tunaunga mkono mipango ya maendeleo kunufaika na mpango huo wa majaribio. Ni azma yetu kuwa baada ya kuwa tumefanya tathmini ya mafanikio na changamoto za hatua hii ya majaribio, tutaupanua mpango huu kushirikisha shule nyingi zaidi kwa kushirikiana na Serikali kwenye mpango wake mkubwa wa kusambaza teknolojia hii katika shule zote za sekondari hapa Tanzania.”
Bwana Ricketts na wataalam wake pamoja na maofisa wa Serikali wameanza kutekeleza mpango huo leo, Jumatatu, Januari 27, 2014, kwa kutoa tabuleti kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wama Nakayama iliyoko Mkoa wa Pwani.
Baada ya leo, shughuli hiyo itahamia Zanzibar na Pemba, kabla ya Bwana Ricketts na wataalam wake kutoa tabuleti kwa shule zilizoko mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Kagera na Morogoro.
Shule zinazonufaika katika mpango huo ni za Serikali na binafsi na kwa kuanzia masomo ambayo yanapatikana katika tabuleti hizo ni hesabu, jiografia, historia na kiingereza.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
27 January, 2014
No comments:
Post a Comment