UPANDE wa serikali katika kesi ya kupinga makato katika kadi za simu umepinga Makampuni ya simu nchini kujiunga katika kesi ya msingi iliyofunguliwa na Taasisi ya Watumiaji wa bidhaa na huduma nchini kote.
Kesi hiyo leo ililetwa mahakamani hapo mbele ya jopo la Majaji watatu ambao ni Lawrence Kaduri, Aloysius Mujuluzi na Salvatory Bongole kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ambapo upande wa serikali ulianza kuwasilisha hoja zao za pingamizi lao la awali.
Akiwasilisha hoja hizo,wakili wa serikali Edson Meyunge alidai kuwa wanapinga kampuni hizo kujiunga katika kesi hio kwasababu hati yao ya kiapo ina makosa kisheria.
Kampuni hizo ni Airtel,Vodacom,Mic Tanzania,Zantel na TTCL. Meyunga alidai kuwa kiapo hicho inaonesha kimeapwa na mtu mmoja (TTCL) hivyo ilipaswa kampuni zinazowakilishwa zioneshe uwakilishwaji wao kwa kusaini katika mkiapo hicho.
"Waheshimiwa majaji ,haya ni maombi ya watu wengi hivyo taratibu zifuatwe,hatuna uhakika kama TTCL ilipewa mamlaka na makampuni mengine kuapa kwa niaba yao"alidai
Akijibu hoya hizo,kwa niamba ya mawakili wengine wa kampuni hizo,wakili Fatuma Karume alidai kuwa pingamizi hilo halina hoja za msingi kwasababu suala la kuthibitisha uwakilishwaji na TTCL ni suala la ushahidi.
Mahakama hiyo imeahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 9 itakapokuja kutoa uamuzi wa pingamizi hilo.
Katika kesi ya Msingi iliyofunguliwa na Taasisi ya Watumiaji wa bidhaa na huduma nchini wanaiomba mahakama hiyo itangaze kwamba sheria iliyopitishwa na Bunge inayotaka kila mtumiaji wa simu ya mkononi kukatwa sh 1,000 kila mwezi ni kandamizi.
Wanadai kwamba watumiaji wengi wa simu za mkononi hawana uwezo wa kukatwa fedha hiyo kwa mwezi, huku wakisisitiza kuwa itawaathiri watumiaji wa huduma hiyo.
Kwa mujibu wa madai ya walalamikaji hao, sheria hiyo inakiuka matakwa ya katiba ya nchi ya uhuru wa kupashana habari na kuiomba mahakama kuifuta sheria hiyo waliyoiita kuwa kandamizi.
No comments:
Post a Comment