MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Kala Jeremiah ameamua kumuenzi aliyekuwa msanii wa hip hop, Albert Mangwea 'Ngwair' aliyefariki Mei 28 mwaka huu nchini Afrika Kusini kwa kutoa tuzo yake aliyoipata mwishoni mwa wiki iliyopita.
Msanii huyo amepokea tuzo za Kilimanjaro Music 2012-2013. ikiwemo ya msanii bora wa hip hop mwaka huu .
Akizungumza na jarida hili, Kala aliweka wazi kuwa ameamua kumpa tuzo hiyo kutokana na heshima aliyokuwa nayo katika suala la muziki hususani wa hip hop .
Alisema anastahili kupewa tuzo hiyo kutokana na uwezo, ambao alikuwanao na isitoshe alianza muziki kabla yake na mazuri ambayo alikuwa anayafanya ndiyo yalichangia yeye kuingia katika tasnia hiyo ya muziki.
"Mimi kama msanii bora wa hip hop kwa mwaka huu, nimeamua kumkabidhi tuzo hii ya msanii bora wa hip hop marehemu Ngwair kwa sababu alikuwa anafanya kazi hiyo ya muziki, ambao na mimi sasa nafanya na isitoshe yeye alikuwa ni mwalimu wangu kwa kile alichokuwa anaimba," alisema Kala.
Aliongezea kuwa tuzo hiyo ataipeleka Morogoro kwa mama yake, Ngwair na pia kuipeleka katika kaburi la msanii huyo, ingawa tuzo hiyo itaishi katika nyumba ya mama yake, huku ikionesha ishara ya kile alichokuwa anakifanya.
Alisema Ngwair alikuwa anastahili kuitwa msanii bora wa hip hop, hivyo anaona ni sahihi kuikabidhi tuzo hiyo kwa familia yake, ikiwa ni moja ya kuenzi mazuri aliyoyafanya.
No comments:
Post a Comment