Thursday, June 20, 2013

DOLCE & GABBANA (D&G) JELA KWA KUKWEPA KODI



Wabunifu wa Kitalian Domenico Dolce (Kulia) na Stefano Gabbana wakifurahia umati wa wadau wa mitindo (hawako pichani) baada ya kuhitimisha maonesho ya mitindo ya nguo kwa msimu wa joto na kipupwe mwaka 2013, maarufu kama 2013 Milan Fashion Week, yaliyofanyika Milan, Itali Septemba 23, 2012.

MILAN: Wakali wa mitindo ya nguo duniani Domenico Dolce na Stefano Gabbana jana walihukumiwa kwenda jela mwaka mmoja na miezi nane kwa kosa la kuficha mabilioni ya fedha kwa lengo la kukwepa kodi.

Wabunifu hao maarufu kama D&G(Dolce and Gabana) ambao umaarufu karibu ulingane na watu maarufu wanao wavalisha nguo zao za ubunifu, hawakuwepo mahakamani jijini Milan, Itali wamekataa makosa hayo.


Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, wabunifu hao wanaweza wasiingie jela kwani wamekata rufaa na kwa utaratibu wa rufaa na mlolongo mzima, wanaweza wasiione jela.

Msoma mashtaka Gaetano Ruta aliomba wafungwe miaka miwili na nusu, lakini jaji akaamua kuahirisha adhabu ya kifungo kwa muda.

Msemaji wa kampuni ya D&G aliahidi kutoa maelezo haraka iwezekanavyo.

Mafanikio ya mitindo ya kisasa na ya kuvutia ya nguo za Dolce na Gabbana (D&G) pamoja na suti zao zilizoshonwa kwa unadhifu wa hali ya juu, ni bidhaa zinzopendwa sana na watu maarufu ulimwenguni ikiwa ni pamoja na Kylie Minogue, Kate Moss and Bryan Ferry na kuwafanya D&G kupanda chati kwa kasi kwenye ulimwengu wa mitindo.

Mwaka 2009, walimualika na kumvalisha mwanamuziki maarufu duniani Madona, katika jumba lao la kifahari lililoko Portofino, Italia. Kesi hiyo ilianza kufuatiliwa na kuchunguzwa mwaka 2008, ilipotolewa orodha ya wakwepa kodi nchini Itali baada ya mdororo wa kiuchumi kuingia Itali.

Lakini mkumbo huo uliowakumba D&G pia umewakumba watu wengi maarufu nchini Itali. Jumatano (jana), jaji alitoa hukumu kufuatia D&G kuuza bidhaa zao kwenye kampuni iliyoko Luxembourg, Gado mwaka 2004 ili kukwepa kulipa kodi na mrahaba wa kiasi cha yuro bilioni 1.



Ubunifu wa D&G unatokana na asili ya uvaaji wa utamaduni wa eneo lililoko kusini mwa Itali katika kisiwa cha Sicily, ambapo Docle alizaliwa mwaka 1958. Dolce alikutana na Gabbana (mwenye miaka 50), wakati wanaishi katika jengo moja huko Milan.

D&G walifanya maonesha ya mavazi yao mara ya kwanza mwaka 1985, nguo zao zilipata umaarufu mwaka 1990 na kuwaingizia kipato kisichopungua yuro milioni 1.5 mwaka 2011.

Wawili hao wamekuwa wakijitetea kuwa hawana hatia.

“kila mtu anajua hatujafanya lolote” Gabbana aliandika kwenye mtandao wa twitter mwezi juni mwaka 2012 baada ya kesi kuanza kusikilizwa.

Lakini Gabbana baada ya kusikia hukumu hiyo aliamua kuweka picha ya mti wenye rangi nyingi kwenye mtandao wa twitter mda mchache baada ya hukumu hiyo.
 


No comments:

Post a Comment