Tuesday, May 21, 2013

PROFESA JAY AELEZEA SABABU ZA KUHAMIA CHADEMA



MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini Joseph Haule 'Profesa Jay jana amejiunga rasmi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Akizungumza sababu zilizomfanya kujiunga na chama hicho Profesa Jay alisema kuwa sera pamoja na harakati za chama hicho ndicho kigezo ambacho kilimvutia na kumshawishi kujiunga na chama hicho.


Alisema kwa upande wake kila siku amekuwa ni mkombozi wa taifa na amekuwa na mikakati mingi ya kuendelea kulikomboa taifa, kwa kutumia muziki wake.

Alisema sera za kukandamizwa, kudidimizwa, kuchochea udini na mambo mengine yasiyofaa hazina tija kwa taifa linaloangalia maendeleo kwa kwa kutumia sera hizo bado kutawagawa wananchi kwa makundi ya walio nacho na wasionacho.

"Mimi ni kama daraja ni mkombozi wa wanyonge hakuna maisha bora kupitia sera za ukandamizaji lakini sera za CHADEMA ni sera ambazo ziko huru na hazifungamani " alisema Profesa Jay

"Hayati Baba wa Taifa alisema kuwa ili tuendelee tunahitaji kuwa na siasa safi, ardhi, watu pamoja na uongozi bora, hivyo ili tuendelee tunahitaji viongozi bora na si bora viongozi" alisema Jay

Profesa Jay aliongezea kuwa hakuna mtu aliyemshawishi kujiunga na chama hicho bali ni maamuzi yake mwenyewe na amepata baraka zote kutoka kwa wazazi wake wote wawili

Alisema kuwa amejiunga kwenye chama hicho ili kuongeza chachu ya maendeleo na ataendelea kukijenga  kwa kufuata sera zilizo bora.

"Sina mpango wa kugombea ubunge ingawa nipo hapo kwa ajili ya kuongeza chachu hivyo kama chama kikiamua sawa naweze kugombea ngazi yoyote ile" alimaliza Profesa Jay







No comments:

Post a Comment