Wednesday, April 03, 2013

KAWE YAGEUKA UWANJA WA VITA, KUFUATIA WANAJESHI KUUA RAIA



 Na Mwandishi Wetu

HALI ya taharuki jana iliwakumba wakazi wa Kawe, Dar es Salaam, baada ya Jeshi la Polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kupiga mabomu ya machozi ili kutuliza vurugu zilizotokea kwenye Kituo cha Polisi Kawe kupinga mauaji ya raia yanayodaiwa kufanywa na wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Jeshi hilo lililazimika kufunga barabara kuanzia saa 11 jioni ambapo maandamano ya wananchi yalishirikisha waendesha pikipiki za bodaboda, baiskeli na bajaji.

Inadaiwa raia huyo ambaye alikuwa mwendesha Bajaji, aliuawa wanajeshi watatu wa JWTZ, ambao walimkodisha na baada ya kufika sehemu waliyokuwa wakienda, walishuka ndipo mmoja kati yao akabaini kuibiwa simu yake ya mkononi.

Juhudi za kuitafuta zilifanyika lakini zilishindikana ndipo wanajeshi hao wakaanza kumsaka mwendesha bajaji huyo waliyemkodi wakiamini ndiye aliyeiba simu hiyo ambapo baada ya kumpata, walianza kumpiga sehemu mbalimbali za mwili hadi kumuua.
 
Baada ya taarifa kulifikia jeshi la polisi kituo cha Kawe, OCS wa kituo hicho na polisi wengine walikwenda eneo la tukio na kukutana na waasamaria wema wakauchukua mwili huo na kufanikiwa kumkamata mmoja wa wanaosemekana ni wanajeshi hao.

Kwa mujibu wa askari mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina kwa madai yeye si msemaji wa polisi, alidai wananchi hawakuridhika hivyo walikwenda Kituo cha Polisi Kawe kwa kuandamana wakidai wapewe mwanajeshi huyo ili walipiza kisasi kwa kumuua.

Vijana walioandamana walikuwa na manati pamoja na mawe ambapo magari yanayopita barabara hiyo yalisimamishwa eneo la Ukwamani na kusababisha wananchi kukimbia.

Mpaka tunakwenda mitamboni, polisi walifanikiwa kufunga barabara hiyo ya Kawe kuanzia eneo la Kanisani hadi Ukwamani. Maji ya kuwasha na mabomu ya machozi yalitumika kutawanya umati mkubwa wa watu katika eneo hilo.

Mbunge wa Kawe Halima Mdee aliwasili kituoni hapo majira ya saa tatu usiku akitaka kujua nini kimetokea na kujaribu kuwasihi wakazi wa Kawe kutulia na kuacha dola ifanye kazi yake.

Imma Matukio ilifanya jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, ili aelezee tukio hilo lakini simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani.

 



No comments:

Post a Comment