Friday, June 08, 2012

KUANDAMANA MARUFUKU LEO


Na waandishi wetu

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku  mandamano yaliyopangwa na waislamu leo kwa madai kuwa Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) linafelisha wanafunzi wa kiislamu.

Maandamano hayo yalilenga kumshinikiza Katibu Mkuu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Joyce Ndalichako, kujiuzulu wadhifa huo.

Akizungumza na waandishi wa Habari Dar es Salaam jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Kamishna wa Polisi  Bw.Ahmed Msangi, alisema jeshi la polisi halioni sababu ya kufanyika maandamano hayo.

Aliruhusu ufanyike mkutano uliopangwa kufanyika leo katika viwanja vya Kidongo Chekundu, jijini Dar es Salaam baada ya swala ya Ijumaa.

Kamanda Msangi alisema awali waislamu hao walidai wanataka kufanya maandamano hayo ili kwenda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi baadaye NECTA ili kufikisha kilio.

Alisema sababu za kuzuia maandamano hayo ni baada ya Jeshi la Polisi kuona ugumu wa kutoa ulinzi, kwani waumini watakuwa wanatokea misikiti mbalimbali iliyopo jijini baada ya swala ijumaa kwenda  viwanja vya mkutano.

Wakati huo huo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt.  Shukuru Kawambwa, ataunda Tume ya watu wanne kuchunguza madai yanayotolewa na waislamu kuhusu kufeli kwa wanafunzi wa dini hiyo  katika somo la Kiislamu, baada ya kutangazwa matokeo ya kidacho cha sita, mwaka huu.

Dkt. Kawambwa alifikia uamuzi huo jana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari. Dkt. Kawambwa alisema mbali ya kutolewa kwa  ufafanuzi wa suala hilo, lakini Serikali imeamua kuunda tume ya kuchunguza suala hilo na kujiridhisha kuhusiana na madai hayo.

"Kumekuwepo na malalamiko na madai ya kufelishwa kwa wanafunzi wa kiislamu katika matokeo yao ya kidacho cha sita ambayo yalitangazwa mapema Mei, mwaka huu, hivyo Serikali inaunda tume ya kuchunguza suala hili licha ya kutoa ufafanuzi kupitia wadau wote wa shule za kiislamu,"alisema Dkt. Kawambwa

Akizungumzia muundo wa Tume hiyo ya uchunguzi, alisema mbali na Wizara yenyewe kuhusika itashirikisha Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA) na  Wakuu wa Shule za Kislamu  ili kupata uhakika wa jambo hilo.

"Nawaomba ndugu zangu waislamu kufuata kile ambacho tumekubaliana na kuacha maandamano ambayo hayana matiki yeyote zaidi ya kuchochea vurugu,"alisema Dkt. Kawambwa.









No comments:

Post a Comment