Friday, June 08, 2012

DKT MWAKYEMBE AIBUA UOZO WA KUTISHA ATCL

Na mwandishi wetu

WAZIRI wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe amefichua uozo wa kutisha ndani ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ambapo kiasi cha dola za Marekani 5,000 zilizolipwa kama bima ya fidia ya ndege iliyopata ajali mkoani Kigoma, iliishia mikononi mwa wajanja, badala ya shirika.

Akizungumza na wafanyakazi wa ATCL jana, Bw. Mwakyembe alisema ufisadi mwingine ni kukodishwa kwa ndege aina ya Airbus na kulipiwa gharama za kukodiwa kwa  miezi sita kabla ya kuja nchini kuanza kazi.

Hata hivyo alisema hata pale ilipowasili  nchini haijawahi kuruka, hivyo kuifanya Serikali iburutwe mahakamani idaiwa deni la sh. bil. 69 zinazotokana na uzembe.

"Baada ya bima kulipa nusu ya dola mil 7 za ajali ya ndege iliyotokea Kigoma, wizara tuliagiza zilipwe moja kwa moja kwenye akaunti ya matengenezo ya ndege, lakini matokeo yake ziliingizwa akaunti ya ATCL... kumbe kuna wajanja waliwaambia wadeni wazichukue," alisema Dkt. Mwakyembe.

Akionekana kukerwa na hali hiyo, Dkt. Mwakyembe alisema wakati Kaimu Mkurugenzi Bw. Paul Chizi, akijua ATCL iko mahututi aliingia mkataba wa kukodisha ndege aina ya Boeing 737-500 inayofanyakazi sasa bila kuhusisha wizara, wala Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

"Niliposikia ATCL inaleta ndege nilimwita Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Omari Chambo, kumuliza akaniambia hana taarifa, nikamwita Bw. Chizi ofisini kwangu afike saa 3 asubuhi, yeye akafika saa 4.30, nilimuliza kama Mwanasheria wa Serikali ana taarifa ya mkataba wa kuleta ndege, akasema anayo, siku ya pili mwanasheria akaniambia hajui chochote," alisema Dkt. Mwakyembe.

Alisema hatua aliyochukua ya kumwondoa wake Bw. Chizi, hakukosea licha ya kutokuwa  na mkataba wa ajira, kwani alistaafu kazi ATCL mwaka 2002 na kulipwa mafao yake yote, hivyo kurudi kwake ilipaswa ioneshwe kwa vielelezo.

Dkt. Mwakyembe alikiri kuwa mkataba wa Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) na ATCL ulikuwa na kasoro, lakini alibainisha kuwa menejimenti ya ATCL ilihusika zaidi na si Serikali kama wafanyakazi wanayodai.

"Siwezi kufanya kazi na watu ambao hawasikii,nitafukuza watu wengi, wapo watu kazi yao kuchunguza kiasi gani kimeingia benki wanakwenda kuwapa taarifa wanaodai shiriki ili fedha zichukuliwe," alisema Dkt. Mwakyembe.

Alisisitiza kuwa Serikali haiko tayari kuona wafanyakazi wanakuwa na kiburi cha kugoma kubadilika kwa nia ya kuongeza ufanisi kwa kuchapa kazi, huku mishahara ikiendelea kutoka wizarani.

Alisema wafanyakazi waliomshtaki kwa wabunge  yupo tayari kujitetea kwa kutumia mwanasheria wa Serikali na kuongeza kuwa kamwe hatishiki na watu hao.

Dkt. Mwakyembe alilishambulia gazeti hili kuandika taarifa za wafanyakazi wa ATCL kupinga uamuzi wa Waziri Mwakyembe kumfukuza kazi Mkurugenzi wao Bw. Chizi kuwa uamuzi huo haukufanyiwa utafiti.

Alisema hataki kujaribiwa bali anaahidi kuunda bodi mpya hivi karibuni ambayo itafanya kazi ya kuhakikisha ATCL inajiendesha yenyewe bila kuleta mzigo serikalini.

Mfanyakazi wa Idara ya Mauzo Bi. Erieth Rutihinda aliomba wafanyakazi wa Wizara na Sekta za Umma kutumia usafiri wa ATCL iki kupatikana faida ya kuendesha shirika hilo.

Mwingine Bw. Gasper Gandu alisema mikataba iliyoitia hasara ATCL ilifanywa bila kupata ushauri wa wafanyakazi ambao walipinga kuingiwa kwani walijua matokeo yake.

Pia aliomba Wizara isaidie kuokoa ATCL na kushirikisha wafanyakazi kila kunapotokea taarifa za kuongeza ufanisi wa  kazi au matatizo ndani ya kampuni.

Dkt. Mwakyembe katika majibu yake aliagiza uongozi kutoa taarifa kutumia ubao wa matangazo na kuahidi kukutana na wafanyakazi wa ATCL kila baada ya miezi mitatu na kuahidi kuilipatia sh. bil. 4.5 alizoomba Hazina ili kutumika kwa shughuli za utendaji na kutengeneza ndege.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya Kepteni Lusajo Lazaro alisema atawashirikisha wafanyakazi kila kunapotokea jambo la kuahidi kufufua shirika hilo.












No comments:

Post a Comment