Wednesday, April 04, 2012

MAMA TUNU PINDA APOKEA MICHANGO YA TAIFA QUEENS

 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MAMA TUNU PINDA APOKEA MICHANGO YA TAIFA QUEENS 
 
MKE WA WAZIRI MKUU Mama Tunu Pinda leo amepokea michango kutoka
kwa wadau mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwa ni mwitikio wa ombi lake kwa
Watanzania kuwaomba waichangie timu ya Taifa ya Netiboli (Taifa Queens) ili iweze
kushiriki Mashindano ya Kombe la Afrika mwezi ujao.
 
Amepokea hundi mbili za sh. milioni 3.4 kutoka kwa
kampuni ya Super Doll ambayo imetoa hundi ya sh. milioni 3.2 na Benki ya
Mkombozi ambayo imetoa hundi ya sh. 200,000/-. Makabidhiano hayo yalifanyika leo
mchana (Jumanne, Aprili 3, 2012) kwenye viwanja vya Sigara, Chang’ombe, ambako
Taifa Queens ilikuwa ikifanya mazoezi.
 
Vilevile, Mama Tunu Pinda amepokea simu ya mtandao wa Zantel
namba 0779-000-808 ambayo imeunganishwa na huduma ya EZY-PESA. Simu hiyo ambayo
imekabidhiwa kwa uongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) inawawezesha
Watanzania kutuma pesa kwenye namba hii kutoka mitandao yote ya simu. 
 
Akikabidhi hundi hiyo, Meneja Mahusiano wa SuperDoll, Bw.
Ramoudh Ally alisema anawaomba Watanzania wengine wajitokeze kumuunga mkono Mama
Tunu Pinda kwa kuichangia timu hiyo ya Taifa ya Netiboli.
 
Naye Meneja Mawasiliano wa Zantel, Bi. Awaichi Mawalla
alitumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kutuma michango
yao kupitia namba hiyo ili heshima ya Tanzania ambayo imepewa jukumu la kuandaa
mashindano ya Kombe ya Afrika isitetereke.
 
Mama Tunu Pinda aliwashukuru wote kwa michango yao na
kuwasihi Watanzania wajitokeze kwa wingi zaidi kuchangia mashindano hayo.
 
Tanzania kupitia CHANETA imepewa heshima ya kuandaa Mashindano
ya Netiboli ya Kombe la Afrika ambayo yanatarajiwa kuanza Mei 8-12, mwaka huu.
Gharama za kuendesha mashindano hayo ni zaidi ya sh. milioni 120.
 
 


No comments:

Post a Comment